Kutoka kulia peomota anayemleta JB, GuyGuy Kiangala, Chaz Baba, Muhonda na Dodo |
Na Mahmoud Zubeiry
MWANAMUZIKI
nguli wa dansi Afrika, JB Mpiana anatarajiwa kuwasili nchini Novemba 26, mwaka
huu kwa ajili ya kupamba uzinduzi wa albamu ya Mashujaa Band Novemba 30, mwaka
huu katika viwanja vya Leaders Club, Dar es Salaam na baadaye katika mikoa ya
Arusha Novemba 28 na Mwanza Desemba 2.
Akizungumza na
Waandishi wa Habari asubuhi ya leo katika ukumbi wa Millennium Business Park,
Kijitonyama, Dar es Salaam, rais wa bendi ya Mashujaa, Charles Gabriel Cyprian ‘Chaz
Baba’, alisema mkali huyo wa dansi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC)
anakuja kundi lake zima la Wenge Musica BCBG.
JB Mpiana
ambaye kwa sasa anatamba na albamu yake ya mpya iitwayo Biloko, anatarajiwa
kupagawisha Watanzania na rap yake mpya iitwayo Amataka Na Punda yaani, Panda Punda,
ambayo kwa Kongo inapendwa ile mbaya.
Chaz Baba
alisema kwamba maandalizi ya onyesho lao yanaendela vizuri kwa ujumla na wanamuziki
wapo tayari kuwapa raha Watanzania siku hiyo.
Chaz Baba alisema
bendi yao itaingia kambini wiki ijayo nje kidogo ya Dar es Salaam, ambako hawataki
kuweka wazi, ili kuwaepushia usumbufu wanamuziki wakati zoezi hilo gumu la
maandalizi ya shoo ya kufa mtu.
Alisema albamu
yao, wanayozindua iitwayo Risasi Kidole
ina nyimbo sita, ambazo ni Risasi Kidole
yenyewe utunzi wake Chaz Baba, Ungenieleza
utunzi wake Raja Ladha, Umeninyima
utunzi wa Freddy Masimango, Hukumu ya Mnafiki
utunzi wake Jado FFU, Kwa Mkweo utunzi
wake Baba Isaya na Penzi la Mvutano,
ambao umetungwa na Masoud Namba ya Mwisho.
Chaz Baba
alisema kama ilivyopangwa, mbali na JB Mpiana, wanamuziki wengine watakaopamba
uzinduzi huo ni MB Dogg, H Baba, Ney wa Mitego na wengineo ambao watajulikana
baadaye.
“Sisi kwa upande
wetu tumejipanga vizuri kuwapa watu burudani ambayo tunajua kwa muda mrefu
wameikosa, Mashujaa tunakuja kushujaa, ushujaa wa kuwaburudisha watu na kukata
kabisa kiu yao,”alisema Chaz Baba.
Alisema wanataka
kufanya shoo ambayo hata JB mwenyewe akiona atakubali kwamba Tanzania kuna bendi
yenye ubora sawa na bendi za kwao, Kongo, ambayo ni Mashujaa.
“Hadi sasa
wapenzi wa muziki hapa Dar es Salaam ambao wamebahatika kuona shoo zetu
wanakiri sisi ndio mabingwa wapya wa muziki wa dansi Tanzania, sasa tunataka
tumdhihirishie hilo na JB Mpiana,”alisema Chaz Baba.
Wakati onyesho
la Dar es Salaam litafanyila Leaders, Mwanza itakuwa kwenye ukumbi wa Villa
Park na Arusha ni Tripple A.