JB Mpiana akizungumza mna Waandishi Dar es Salaam leo |
Na Prince Akbar
MWANAMUZIKI
nguli wa dansi Afrika, JB Mpiana ametua jijini Dar es Salaam juzi tayari kwa
maonyesho kadhaa, likiwamo lile la uzinduzi wa albamu ya Mashujaa Band
inayokwenda kwa jina la Risasi Kidole, litakalofanyika Ijumaa katika viwanja
vya Leaders Club, Dar es Salaam.
Kabla ya
shoo hiyo ya Ijumaa, JB Mpiana ambaye amekuja na kundi lake zima la Wenge
Musica BCBG, likiwahusisha wanamuziki wake za zamani na wapya, atauwasha moto
jijini Arusha kesho kabla ya kufanya kweli jijini Mwanza Jumapili.
Akizungumza katika
Hoteli ya Double Tree iliyopo Masaki, Dar es Salaam, JB Mpiana ameahidi kutoa
shoo ya aina yake ambayo anaamini itakonga nyoyo za Watanzania.
Alisema kuwa
amefurahisa sana kuja Tanzania kwa mara nyingine, ikiwa ni pamoja na mapokezi
aliyoyapata, akiahidi kutoa burudani ya nguvu kwa Watanzania kuwalipa mapokezi
waliyomwonesha.
“Nina imani waandaaji wamefanya maandalizi ya
kutosha, nimekuja na wanamuziki wangu wote 25, nimekuja na vifaa vyangu vyote
vilivyopo katika kundi langu, ili kutoa burudani ya kutosha kwa Watanzania.
“Nimewaletea albamu inayojulikana kwa jina la
Biloko (chakula), watanzania wajiandae kula, yaani kupata burudani ya nguvu
kutoka kwangu na kundi langu,” alisema JB Mpiana.
Kati ya
wasanii aliokuja nao, alisema wapo wale wa zamani aliokuwa nao enzi hizo ndani
ya kundi lake hilo lilipoanza kutamba katika anga ya muziki, na wengine wapya
ambao wapo fiti.
Katika
programu yake hapa nchini, amesema atapiga nyimbo zake za zamani na mpya ili
kuwapa watanzania fursa ya kupata vionjo vya zamani na vipya, kuweza kupima
ubora wa kazi hizo.
Akizungumzia
muziki wa Tanzania, amewataka wasanii wa hapa nchini kujituma na kuzipenda kazi
zao na kuiheshimu waweze kufanikiwa katika kazi zao hizo.
Juu ya
kiongozi wa safu ya unenguaji, alisema safari hii inaongozwa na mwanadada
Zambrota, ikiwa ni baada ya kufariki kwa aliyekuwa akishikilia nafasi hiyo,
Monica.
“Nimefurahi sana kuja Tanzania kwa mara
nyingine, wapenzi wa burudani wajiandae kupata shoo ya nguvu kutoka kwa JB
Mpiana,” alisema mkali huyo.
Kwa upande
wake, Mkurugenzi wa kampuni ya QS Muhonda, Joseph Muhonda, waratibu wa maonesho
hayo, amesema kuwa ni matarajio yao wakazi wa Dar es Salaam, Arusha na Mwanza,
watafurahia shoo hiyo kutoka kwa JB Mpiana na Mashujaa kutokana na maandalizi
ya nguvu waliyofanya, akiwataka wakazi wa maeneo hayo, kujitokeza kwa wingi.
Alisema kuwa
katoka onesho la JB Mpiana jijini Arusha, atatumbuiza katika ukumbi wa Triple A
kuanzia saa tatu usiku, wakati Desemba Mosi atakuwa katika ukumbi wa Villa Park
kuanzia saa tatu usiku.
“Maandalizi yote yapo sawa, kila kitu
kimekamilika, tuliahidi JB Mpiana anakuja na kweli amekuja kama mlivyomuona,”
alisema na kuongeza kuwa JB Mpiana atasindikizwa na wasanii wa Bongo Fleva kama
H Baba, MB Doggy, Ney wa Mitego na wengineo.