IMEKUWA bahati kwa mshambuliaji chipukizi wa Coastal Union, Atupele Green Jackson ambaye ameibukia Ligi Kuu Bara msimu huu kwa mara ya kwanza na kuwamo kwenye 'First 11' ya kikosi chake.
Atupele alisajiliwa na Coastal akitokea Yanga B na amepata bahati ya kuaminika kikosini na kuwa chaguo la kwanza la kocha Ahmed Morocco.
Nyota huyo mweusi, mrefu na ana umbo kubwa linalomfanya ajiamini na kuwa 'sumu' kwa mabeki wasumbufu.
Wataalamu wa soka nchini wanadai atakapopata uzoefu atakuja kuwa tishio na kulisaidia Taifa la Tanzania.
Kutokana na umbo lake watu humfananisha na Mtanzania, Thomas Ulimwengu anayekipiga Klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri Kidemokrasi ya Congo na wako wote katika timu ya taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 20, 'Ngorongoro Heroes'.
Ametua Coastal kwa mkataba wa miaka mitatu na kwa kipindi kifupi ameonyesha uwezo wa juu katika mechi alizocheza, lakini amekumbwa na tatizo la ukame wa mabao kwani hadi sasa bado hajaziona nyavu lakini yeye anasema ni hali ya kawaida na anaamini utafika wakati wake atafunga.
Mwanaspoti lilifanya mahojiano naye kwa kirefu na anafafanua kwa undani, siri ya mafanikio, historia na malengo ya maisha yake kwa ujumla.
Sababu ya kuaminiwa
"Nafikiri ni kujituma na ushirikiano wangu mzuri na wachezaji wenzangu lakini pia kufuata maelekezo ya mwalimu," anasema Atupele anayevutiwa na nyota Didier Drogba wa Ivory Coast, Mghana Asamoah Gyan na Mbrazil Ronaldo de Lima wakati Tanzania anamhusudu Haruna Moshi 'Boban'.
Kuhusu kukosa mabao, Atupele anasema: "Sina wasiwasi kwa sababu utafika wakati wangu nami nitafunga.
"Usipofunga unaumia kujiuliza maswali mengo lakini ni hali ya mchezo tu lengo ni kuisaidia timu ifanye vizuri."
Kocha wake, Ahmed Morocco anamzungumzia mchezaji huyo kuwa ni mzuri ndiyo maana anamtumia: "Mchezaji mzuri na muhimu kikosini, kuhusu kufunga tumpe muda."
Nje ya soka
Atupele anasema anapokuwa hana majukumu na soka anapenda kuutumia muda wake mwingi kuendesha gari.
"Napenda sana kuendesha gari na ndiyo furaha yangu ninapokuwa nje ya kazi za mpira," anaeleza.
Pamoja na kupenda kuendesha gari, Atupele anaongeza kuwa bado hajanunua la kwake binafsi na mara nyingi hutumia la rafiki yake, Kiggi Makassy anayekipiga Simba.
Hata hivyo, mpango wake kama mambo yake yataenda vizuri, malengo yake ni kununua gari.
Alifanyiwa usaili na Kondic
Kinda huyo anasema kipaji chake ni cha tangu utotoni na alipata umaarufu akiwa Shule ya Msingi ya Lugalo.
Ni zao la shule ya vipaji ya Global Soccer Academy ambayo ilianzishwa na Wazungu na walikuwa wanadhaminiwa na Kampuni ya simu za mikononi ya Vodacom.
Alijiunga na kituo hicho akiwa mwanafunzi wa Shule ya Kambangwa kabla ya kutua Yanga.
Alichaguliwa na Yanga baada ya kufanyiwa usaili na kocha wa zamani wa Yanga, Mserbia Dusan Kondic.
"Nilijiunga Yanga baada ya kufanyiwa usaili na kocha Kondic. Tulichukuliwa vijana wote tukaunganishwa na Yanga B tukacheza mechi na timu ya wakubwa nikafanya vizuri na ndipo nikachaguliwa," anaongeza.
Atupele anasema alishawishika kujiunga na Yanga baada ya ushauri kutoka kwa rafiki yake aliyemtaja kwa jina la Hamad Kibopile, ambaye pia alikuwa anaichezea Yanga B.
"Yeye alikuwa anachezea Yanga B na aliponiona Globo akanishawishi nijiunge na Yanga."
Sababu ya kuondoka Yanga
Atupele alihamia Coastal Union baada ya kutofautiana na Yanga kwa masuala ya mkataba.
"Nilihama Yanga baada ya kutofautina kwenye masuala ya mkataba nami ni mchezaji nikaamua kuja kutafuta maisha,"anasema Atupele na kugoma kuongelea kwa undani.
Hata hivyo, licha ya Atupele kutoingia kwa undani kuhusu suala hilo, Mwanaspoti linafahamu kuwa mtafaruku wao ulisababishwa na fedha za usajili kutokwenda sawa na makubaliano waliyopatana.
Atupele aliona pesa hiyo haitoki kama walivyopatana licha ya kuwa tayari alishasaini mkataba kwa ajili ya msimu huu wa 2012-2013 wa Ligi Kuu Bara na alipodai Yanga wakaona isiwe tabu wakamalizana kwa kuuchana.
Atupele ameenda mbali na kusema, endapo Yanga itamhitaji kwa mara nyingine hana tatizo wakikubaliana na uongozi wake kwani anachoangalia ni maslahi.
Anavyoizungumzia Coastal na Taifa Stars
"Coastal ni bora na ina malengo kwenye ligi hii na mambo yakienda sawa tunaamini tutamaliza tukiwa katika nafasi tatu za juu."
Safu ya ushambuliaji ya Coastal ina matatizo baada ya kuwakosa Nsa Job, ambaye ni majeruhi wa mguu pamoja na Pius Kisambale aliyefanyiwa upasuaji.
"Ni pengo kuwakosa wachezaji mliozoeana kucheza kitimu lakini wapo wengine wataziba mapengo."
Historia
Atupele amezaliwa katika familia yenye watoto watano na yeye ni wa nne. Mama yake, Doto Ludete alimzaa yeye pamoja na ndugu zake Kassim, Asha, Abdallah na Tatu.
Atupele amefafanua sababu ya kutofautiana majina na ndugu zake hao kuwa imechangiwa na kuwa na mama na baba tofauti.
Alisoma shule ya Msingi Lugalo na kumalizia Sekondari ya Kambangwa. Hajaoa na hana mtoto.
ATUPELE GREEN JACKSON
Amezaliwa: Agosti 30,1994
Mahali: Lugalo, Dar es Salaam
Klabu: Yanga 'B' 2009-2012,
Coastal Union 2012-
Taifa: Tanzania
IMEHAMISHWA: Kutoka gazeti la Mwanaspoti