MARA kadhaa
nimeandika juu ya umuhimu wa kuwekeza katika soka ya vijana, ili kutengeneza
msingi wa timu bora ya taifa ya baadaye.
Na Mahmoud Bin Zubeiry |
Kwa wasomaji
wangu wazuri, bila shaka watakuwa wanakumbuka namna nilivyokuwa nashauri kuhusu
maandalizi ya timu ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 17, Serengeti Boys
tangu hata Kenya na Misri hazijajitoa.
Pamoja na
uzito wa viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hatimaye dakika za
mwishoni wakafanikiwa kuiwekea mikakati timu hiyo, kwa kuiundia Kamati Maalum
ya kuisaidia, chini ya Mwenyekiti, Ridhiwani Kikwete na Wajumbe kama Kassim
Dewji, Abdallah Bin Kleb, Seif Ahmad Magari, Nassor Bin Slum, Salim Abdallah na
wengineo.
Katika
kipindi kifupi cha kuundwa kwake, Kamati hiyo imeonyesha ufanisi na hadi leo
Serengeti Boys inaingia kwenye mchezo wa kwanza wa Raundi ya tatu na ya mwisho
dhidi ya Kongo Brazzaville Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, kuna matumaini.
Yapo
matumaini ya timu hiyo kukata tiketi ya kucheza Fainali za U17 Afrika mwakani
nchini Morocco.
Juzi,
nilihudhuria hafla ya chakula cha usiku cha kuchangia timu hiyo, ambayo hata
hivyo haikufanikiwa kutokana na kuchelewa kwake kuanza, wadau wengi walioalikwa
waliondoka baada ya kuona muda walioambiwa shughuli itaanza unazidi kuyoyoma na
hakuna dalili za kuanza kwake.
Lakini
angalau unaweza kuona Wajumbe wanafanya kazi ndani na nje ya Uwanja,
kuhakikisha timu hiyo inafuzu.
Hakuna
asiyefahamu kwamba nyumba bora inatokana na msingi wake imara- hivyo hata soka
ya Tanzania, inatakiwa kujengewa msingi imara, ambao ni kuwekeza kwenye soka ya
vijana.
Jamani,
kuwekeza kwenye soka ya vijana si tu kuanzisha vituo au timu za vijana, bila
kuwa na mikakati ya kuwaendeleza vijana wenyewe hatua kwa hatua.
Tustaajabu
kwa nini Tanzania haijacheza tena Fainali za Mataifa ya Afrika tangu ilipofuzu
kizalizali mwaka 1980, ikiwa hatuna msingi imara wa soka ya vijana?
Lazima
tuzoeleke kwenye Fainali za Afrika za Vijana, ili tufikirie kucheza Fainali za
wakubwa.
Niliwahi
kutoa mfano mdogo tu; Mchezaji anapigiwa wimbo wa taifa akiwa kwenye fainali za
vijana za Afrika, tarajia huyo lazima atatamani kupigiwa wimbo huo na kwenye
fainali za wakubwa pia.
Juzi, maneno
ya Nahodha wa Serengeti, Miraj Adam na Msaidizi wake, Hussein Twaha yalionyesha
dalili hizo, vijana wamefurahia hadhi tu waliyopewa kwa kuundiwa Kamati ya
kuwasapoti na wameahidi kuifunga Kongo leo.
Wamehamasika,
tayari wana hamu na kitu. Lakini kama wangetelekezwa tu kama ilivyokuwa, bila
kuonyeshwa kwamba kuna watu wapo nyuma yao, leo dhamira ingekuwa kushindana kwa
uwezo na nguvu zao zote, au kucheza kutimiza wajibu?
Soka yetu
inazidi kuporomoka kila kukicha- leo Tanzania ni ya 134 kwa ubora katika
viwango vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), yaani hata katika ukanda
wetu wa CECAFA, tunazwazidi Somalia (193), Sudan Kusini (200) na Eritrea tu
(192), lakini nchi nyingine zote, Uganda (86), Ethiopia (102), Sudan (102), Rwanda
(122), Burundi (128) na Kenya 130 zinatuzidi.
Tangu Jakaya
Kikwete aingie Ikulu, tumekwishabadilisha walimu watatu wa kigeni, Mbrazil
Marcio Maximo ambaye chini yake tulikosa fainali mbili za Afrika, zilizofanyika
Ghana 2008 na Angola 2010, Mdenmark Jan Borge Poulsen ambaye chini yake
tulikosa tiketi ya Gabon na Equatorial Guinea na huyu wa sasa Kim Poulsen,
ameshindwa kutupa tiketi ya Afrika Kusini mwakani.
Hakuna
matarajio ya mabadiliko makubwa hata baada ya miaka 20 ijayo, iwapo staili
zitaendelea kuwa hivi hivi na umefika wakati sasa tukakubali kujiwekea dira
mpya ya muda mrefu.
Lazima
tukubali kuwekeza gharama katika kuwaandaa wachezaji kwa muda wa kutosha, ili
baadaye tuwe na timu nzuri ya taifa, timu ya ushindani.
Mara kadhaa
nimekuwa nikirudia kushauri juu ya umuhimu wa kuzishirikisha timu zetu za
vijana kwenye mashindano ya kimataifa kwa ukamilifu, lakini bado wahusika
hawajaona umuhimu wa hilo.
Kwa sasa Tanzania
kuna mashindano mengi ya vijana ambayo yanasaidia kuibua vipaji, lakini tatizo
hakuna mfumo wa kuwaendeleza hao vijana, matokeo yake inakuwa sawa na mkulima
anayepanda mazao yake, lakini anashindwa kuyatunza, je, huyo atavuna kweli?
Hicho ni kilimo cha aina yake.
TFF
wanapaswa kutenga bajeti na mikakati madhubuti kwa ajili ya timu za vijana
chini ya umri wa miaka 17, 20 na 23 - kwani hilo ndilo chimbuko la kuwa na timu
bora ya taifa baadaye.
Nitatoa
mfano; Julai 8, mwaka 2001, Ghana iliingia fainali ya Kombe la Dunia kwa vijana
chini ya umri wa miaka 20 na ikafungwa 3-0 na Argentina kwenye Uwanja wa Jose
Amalfitani mjini Buenos Aires, mabao ya Diego Colotto dakika ya sita, Javier
Saviola dakika ya 14 na Maxi Rodriguez dakika ya 73.
Kikosi cha
Ghana siku hiyo kilikuwa; Maxwell Banahene, Sulley Muntari, Michael Essien,
Patrick Villars, Emmanuel Pappoe, Ibrahim Abdul Razak, Razak Pimpong
aliyempisha Frank Osei dakika ya 75, Derek Boateng, John Mensah, John Pantsil
na Kwaku Duah, aliyempisha Samuel Thompson dakika ya 68.
Mwaka 2006
tukashuhudia asilimia kubwa ya vijana hao na wengine walioibuliwa baadaye
wakiiwezesha Ghana kukata tiketi ya kucheza fainali za Kwanza za Kombe la Dunia
nchini Ujerumani.
Oktoba 6,
mwaka 2009, Ghana ilitwaa Kombe la Dunia la vijana chini ya umri wa miaka 20,
ikiifunga Brazil katika fainali kwa mikwaju ya penalti 4-3, baada ya dakika 120
za bila kufungana, kwenye Uwanja wa Cairo International, Cairo.
Kikosi cha
Ghana kilichoweka rekodi ya kuwa nchi ya kwanza ya Afrika kutwaa ubingwa wa
michuano hiyo, kilikuwa; Daniel Adjei, Samuel Inkoom, Jonathan Mensah, Daniel
Addo, David Addy, Abeiku Quansah aliyempisha Opoku Agyemang dakika ya 107,
Emmanuel Agyemang-Badu, Nahodha Andre Ayew, Mohammed Rabiu aliyempisha
Bright Addae
dakika ya 101, Ransford Osei aliyempisha Ghandi Dassenu dakika ya 65 na Dominic
Adiyiah.
Tumeona
mwaka juzi, mseto wa nyota walioifikisha fainali ya U20 Ghana na walioipa
ubingwa wa michuano hiyo 2009 Misri, ukiifikisha timu ya wakubwa ya nchi hiyo
Robo Fainali ya Kombe la Dunia.
Ghana
ingeweza kuweka historia ya kuwa nchi ya kwanza kufika Nusu fainali, kama si
refa Mreno Olegario Benquerenca kutoa uamuzi wa utata, baada ya Luis Suarez wa
Uruguay kuupangua mpira uliokuwa tayari nyavuni.
Nimetoa
mfano kwa Ghana, kwa sababu ndio ambao kwa miaka ya karibuni wamevuna matunda
ya kuwekeza kwenye soka ya vijana- lakini kwa ujumla nchi zote duniani zilizo
makini katika soka zinatilia mkazo soka ya vijana.
Sasa Mungu
katusaidia, tumepata sehemu ya kutengenezea msingi imara, ambao ni kuhakikisha
Serengeti inakwenda Morocco mwakani. Binafsi nimefurahi sana na ninatarajia
furaha zaidi kuanzia leo kutoka kwa vijana hao. Tujitokeze kwa wingi kwenda
kuwashangilia vijana, ili kuwapa hamasa washinde. Mungu ibariki Tanzania. Amin.