Joseph Owino anarudi nyumbani Msimbazi |
Na Mahmoud Zubeiry
AZAM FC
wanataka Sh. Milioni 10 pamoja na kiungo Uhuru Suleiman kutoka Simba, ili
wawape beki Mganda Joseph Owino.
Habari za
ndani, ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka Azam, zinasema kwamba tayari
makubaliano yamefikiwa lakini, Simba inaonekana kusuasua kutekeleza makubaliano
hayo.
Azam wanadai
wamekubaliana na Simba walipe fedha hizo Sh Milioni 10 na kumuidhinisha Uhuru
kuhamia Chamazi, lakini suala la fedha bado halijatekelezwa.
“Tena hapo
bado kuna kesi ya fedha nyingine, Sh. Milioni 5, ambazo Simba wanadaiwa na
Uhuru, sisi tumekubali kumpa fedha hizo Uhuru, halafu wao tutawakata kwenye mapato
ya mlangoni katika mechi yetu na wao ya marudiano,”kilisema chanzo kutoka Azam.
Lakini upande
wa Simba nao wanasema fedha zote, Sh Milioni 15 walikubaliana zikatwe katika mapato
ya milangoni.
Simba
imeamua kumrejesha Owino, ili kuimarisha safu yake ya ulinzi, ambayo imeonekana
kuyumba katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Lakini pia
hiyo ni nafuu kwa beki huyo Mganda, ambaye ameshindwa kupata namba kwenye
kikosi cha kwanza cha Azam chini ya makocha wote, kuanzia Mserbia Boris Bunjak
aliyefukuzwa na huyu wa sasa Muingereza, Stewart Hall aliyerejeshwa kazini.