Hayatou kushoto akiwa na Rais wa FIFA, Sepp Blatter kulia |
Na Mahmoud Zubeiry
RAIS wa
Shirikisho la Soka Afrika (CAF), Issa Hayatou amekubali kuhudhuria sherehe za
ufunguzi wa michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, Cecafa-Tusker
Challenge wiki ijayo mjini Kampala, Uganda.
Ofisa Habari
wa Shirikisho la Soka Uganda (FUFA), Rogers Mulindwa ameiambia BIN
ZUBEIRY leo kutoka Uganda kwamba, Baraza la Vyama vya Soka Afrika
Mashariki na Kati (CECAFA) tayari limepokea uthibitisho wa Hayatou kufungua
michuano hiyo kutoka makao makuu ya CAF, Cairo, Misri.
Bosi huyo wa
soka barani, anatarajiwa kuwasili Kampala Novemba 22, kufuatia mwaliko huo wa
Rais wa CECAFA, Leodegar Tenga.
Rais wa FUFA,
Lawrence Mulindwa amesema Uganda imefurahia heshima hiyo ya ujio wa Hayatou,
ambaye atafuatana na viongozi mbalimbali wa CAF, akiwemo Katibu Mkuu, Hicham El
Amrani, Mohamed Raouraoua, Constant Omari na Ngangue Appolinaire. Katika ziara
yake hito, Hayatou atahudhuria Mkutano wa CECAFA katiuka hoteli ya Serena Ijumaa
ya Novemba 23 kabla ya kufungua rasmi michuano ya mwaka huu ya Cecafa-Tusker
Cup Uwanja wa Namboole jioni ya siku inayofuata.
Uganda itawakaribisha
jirani zao Kenya katika mchezo wa ufunguzi wa michuano hiyo saa 10:00 jioni, Jumamosi
ya Novemba 24.