Na mahmoud Zubeiry
KAMATI ya
Utendaji ya klabu ya Simba ya Dar es Salaam inatarajiwa kuwa na kikao kizito
leo, kujadili mambo mbalimbali kuhusu mustakabali wa klabu hiyo na mwenendo wa
timu yao ya soka kwa ujumla.
Habari
kutoka ndani ya Simba, zimesema kwamba kikao hicho kitashirikisha Wajumbe wote
wa Kamati hiyo, chini ya Mwenyekiti wake, Alhaj Ismail Aden Rage.
Miongoni mwa
ajenda zinazotarajiwa kuwa mjadala mzito na matokeo ya timu hiyo kushika nafasi
ya tatu katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, licha ya kuanza vema na kufikia
kuongoza kwa wastani wa pointi saba zaidi.
Aidha,
katika kikao hicho, habari zinasema Makamu Mwenyekiti, Geoffrey Nyange ‘Kaburu’
atawasilisha rasmi barua ya kujiuzulu kwake uongozi, kufuatia kuibuka watu
wanaompinga na kushinikiza ajiuzulu.
Lakini pia
bado mjadala mpana utakuwa kuhusu mustakabali wa timu kuelekea mzunguko wa pili
wa Ligi Kuu na michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika. Litajadiliwa suala la kipa
Juma Kaseja kuomba kung’atuka baada ya kufanyiwa fujo na mashabiki.
Litajadiliwa
suala la kusimamishwa kwa beki Juma Said Nyosso na kiungo Haruna Moshi ‘Boban’.
Litajadiliwa suala la kuboreshwa kwa timu kuelekea mzunguko wa pili wa Ligi Kuu
na Ligi ya Mabingwa mwakani.
Lakini pia
habari zinasema litajadiliwa pendekezo la kutaka kocha wa timu hiyo, Mserbia
Profesa Milovan Cirkovick aondolewe na masuala mengine ya msingi, kama salio la
malipo ya kiwanja, ambacho klabu hiyo inataka kujenga uwanja wake wa
michezo.
Kwa ujumla,
hamkani si shwari ndani ya Simba hivi sasa, baada ya mabingwa hao wa Ligi Kuu
kumaliza mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu wakiwa katika nafasi ya tatu, tena
wakizidiwa pointi sita na wapinzani wao wa jadi, Yanga wanaoongoza ligi hiyo.