Mwenyekiti wa F.O.S., Zacharia Hans Poppe |
Na Mahmoud Zubeiry
KUNDI la Friends
of Simba (F.O.S.) linatarajiwa kukutana leo jioni kujadili mustakabali wa klabu
kwa ujumla na kutoa msimamo wao mbele ya wanachama na wapenzi wa klabu hiyo.
Hamkani si
shwari Simba kwa sasa baada ya timu kumaliza nafasi ya tatu katika msimamo wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, ikitoka kuongoza kwa wastani wa pointi saba.
Mwenyekiti
wa F.O.S., Zacharia Hans Poppe ameiambia BIN ZUBEIRY juzi kwamba, watakuwa na
Mkutano kesho kujadili hali ya mambo klabuni kwao.
“Sisi kazi
yetu ni kusapoti uongozi uliopo madarakani, kuhakikisha timu yetu inafanya
vizuri, sasa hali inayoendelea sasa inatutia shaka kuelekea mwakani, ambako
tutakuwa na mtihani wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na pia Ligi ya Mabingwa.
Kwa hivyo
tutakutana, tutazungumza kwa mapana marefu sana, ili tujue undani na ukweli wa
matatizo yaliyopo klabuni na baada ya hapo na sisi tutatoa mtazamo
wetu,”alisema kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Baada ya
kumalizika kwa mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu, Kamati ya Utendaji ya Simba,
chini ya Mwenyekiti wake, Alhaj Ismail Aden Rage ilikutana na kufikia maamuzi
ya kuvunja Kamati zote ndogondogo za klabu pamoja na kulifuta tawi la wanachama
wakorofi, Mpira Pesa la Magomeni, waliomtukana kipa Juma Kaseja na kuendesha
harakati za mapinduzi.
Lakini pia
wasiwasi umeingia kutokana na kuvunjwa pia kwa Kamati ya Usajili, iliyokuwa
chini ya Mwenyekiti Hans Poppe katika kipindi hiki kigumu ambacho klabu
inatakiwa kurekebisha usajili kuelekea mzunguko wa pili na Ligi ya Mabingwa.
Mbali na
hivyo, kuna suala la mchezaji Emanuel Okwi ambaye amemaliza mkataba wake kwenye
klabu hiyo na alikuwa kwenye majadiliano na Kamati ya Usajili, ambayo yalifikia
pazuri, lakini kwa kuvunjwa kwa Kamati hizo, maana yake mazungumzo hayo
hayawezi kuendelea. Mshambuliaji Mzambia, Felix Sunzu Jr. pia naye
anamaliza mkataba wake mwezi ujao.