Na Princess Asia
KAMPUNI ya fastjet,
Shirika la ndege la kwanza Afrika la nauli nafuu, leo limezindua mauzo ya
tiketi zake nchini Tanzania, ikiwa ni maandalizi ya safari yake ya kwanza ya
kibiashara mwishoni mwa mwezi huu.
Uzinduzi huo wa tiketi ni hatua muhimu katika
juhudi za kampuni kuwezesha usafiri wa ndege kwa Watanzania wako wengi ambao
awali walikuwa hawamudu gharama za safari za ndege. Huku nauli za anga zikiwa
zinaanzia Tsh32, 000 (U$D20) kabla ya kodi za serikali, usafiri wa anga sasa
unakuwa moja ya njia nafuu za watu kusafiri.
fastjet, ambayo imeinunua Fly540, imechagua Dar
es Salaam kuwa kituo chake cha kwanza cha uendeshaji barani Afrika, huku safari
za ndege zikiwa zimepangwa kuanza kuruka kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa
Julius Nyerere kuanzia Novemba 29. Tiketi za Dar es Salaam – Kilimanjaro na Dar
es Salaam – Mwanza zinaanza kuuzwa kuanzia leo. Safari zingine, za ndani na
kanda ya Mashariki mwa Afrika, zitaanza baada ya wiki kadhaa.
Akizungumzia uzinduzi wa mauzo ya tiketi,
Afisa Mtendaji Mkuu wa fastjet, Ed Winters alisema:
“Hiki ni kipindi cha kihistoria kwa safari za
anga Tanzania, na hasa Afrika. Usafiri wa anga siyo tena himaya ya watu
wachache Tanzania. fasyjet itafanya usafiri wa anga kuwa kitu ambacho
Watanzania wengi wanakimudu tofauti na awali, na hivyo kutoa fursa nzuri zaidi
kwa biashara, safari za likizo, na wanafamilia kutembeleana. Tunawashukuru
wabia wetu Tanzania kwa ushirikiano wao mpaka leo hii, na tunamatumaini ya
uhusiano mrefu na wenye manufaa kwa watanzania.”
Tiketi zinapatikana kupitia mawakala wa usafiri
na dawati la mauzo, kituo cha mawasiliano na ofisi za fastjet yenyewe. Tovuti
mpya ya fastjet, www.fastjet,com itazinduliwa wiki ijayo na kutoa taarifa za
safari na nauli. Tovuti hiyo pia itaruhusu kununua tiketi kwa kutumia kadi za
credit/debit pamoja na simu za mkononi.
Uzinduzi
wa Chapa ya fastjet
Fastjet pia imezindua chapa yake mpya kabla ya
kuanza kwa safari zake za kibiashara. Nembo ya
kampuni ni kasuku (kasuku wa kijivu wa Afrika) ambaye alichaguliwa
kutokana na sifa zake za maarifa, urafiki na kuakisi kaulimbiu ya fastjet ambayo
ni usafiri wa akili. Wiki hii pia itashuhudia uzinduzi wa mtandao wa kijamii wa
fsaftjet kupitia Facebook na Twitter na hivyo kutoa ukumbi kwa wateja na wadau Kuwasiliana
na kuchangia mawazo yao kuhusu kampuni kwa njia ya mtandao.
Richard Bodin, Afisa Biashara Mkuu wa fastjet
anasema:
“Moja ya hulka kuu za fastjet ni uwazi.
Tunataka kuziba pengo kati ya mlaji na shirika la ndege kwa kuhakikisha
tunakuwa na mawasiliano ya pamoja kila inapowezekana na kusikiliza mahitaji na
vipaumbele vya wateja. Mitandao ya kijamii ni njia bora ya kufanikisha hili –
kumbi kama Facebook na Twitter hutuwezesha kuwasiliana moja kwa moja na wateja
na kutusaidia sisi kuelewa vizuri zaidi na kuiwezesha fastjet kwenda sambamba
na mahitaji na mapendeleo ya wadau wetu.
Shirika lina ndege tatu za kisasa aina ya
Airbus A319. Ndege zote tatu zimo kwenye mchakato wa kupakwa rangi na nembo za
fastjet kabla ya kuletwa Tanzania tayari kwa uzinduzi wa safari za kibiashara
baadae mwezi huu.
Kuhusu fastjet Plc
fastjet Plc ni kampuni mama ya Shirika la
Ndege la Afrika Fly540, ambalo hujiendesha kutoka vituo vinne Kenya, Tanzania,
Ghana na Angola. Kwa sasa Fly540 ina ndege 10 zenye kuhudumia kama njia 25 za
ndani na kanda, ikibeba takriban abiria 750,000 kwa mwaka, huku ikiwa na
msisitizo mkubwa kwenye usalama, ulinzi na kuaminika.
Baada ya mashauriano na mwanzilishi wa
easyjet, Sir Stelios Haji-Ioannou, kampuni ya easyGroup ililenga kubaini
uwezekano wa kuwa na shirika la ndege la nauli nafuu Afrika, kama ilivyo Ulaya,
na hivi sasa tunajiandaa kuzindua fastjet, shirika la kwanza la ndege Afrika la
nauli nafuu, likiwa na ndege za kisasa kwa kutumia leseni na njia za Fly540.
Safari za kwanza kwa kutumia chapa ya fastjet zinatarajiwa kuanza mwishoni mwa
Novemba, na hivyo kuja na aina mpya kabisa ya safari za anga kwenye soko la
Afrika.
fastjet Plc imeorodheshwa kwenye Soko la Hisa
la London (LSE). Kwa maelezo zaidi, tembelea www.fastjet.com