Didier Kavumbangu akishangilia moja ya mabao aliyoifungia Yanga katika mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu |
Na Mahmoud Zubeiry
WAKATI mwingine ipo haja ya kukubali ushauri wa kitaalamu,
kuwaachia walimu wafanya usajili. Bila shaka katika michuano ya Klabu Bingwa
Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame Julai mwaka huu Dar es Salaam, Didier
Kvumbangu pamoja na kuwafunga Yanga akiwa Atletico ya Burundi jina lake halikuvuma
sana kwa sababu hata timu yake haikufanya vizuri sana.
Kavumbangu aliwafunga Yanga mabao mawili, wakilala 2-0 katika
mchezo wa kwanza wa makundi wa Kagame na zaidi ya hapo, Yanga haikufungwa tena
hadi inachukua ubingwa.
Lakini mabao ya Didier hayakuchukuliwa kama yalitokana na
umahiri wa ufungaji, hapana- bali yalichukuliwa kama ya bahati na pia kuikuta
timu hiyo ikiwa haiko sawa kutokana na kuundwa na wachezaji wengi wapya.
Hata hivyo, mwisho wa msimu Yanga ilipoona inahitaji kuongeza
nguvu katika safu ya ushambuliaji, viongozi waliomba kocha wa timu yao wakati
huo, Tom Saintfiet awapendekezee jina la mchezaji kutokana na michuano hiyo ya
Kagame.
Mtakatifu Tom aliwashangaza sana viongozi wa Yanga kwa
kuwatajia mchezaji aliyewafunga mabao mawili katika mechi ya kwanza, wakati
kuna wachezaji wengine wanang’ara kutoka klabu za AS Vita ya Jamhuri ya
Kidemokrasia ya Kongo (DRC), APR ya Rwanda na nyinginezo.
Uzuri tu viongozi wa Yanga walikubaliana na ombi la kocha huyo
Mbelgiji na wakamleta mshambuliaji huyo Dar es Salaam. Awali, kidogo ulitaka
kuanza kujitokeza wasiwasi juu ya mchezaji huyo kutokana na kuchelewa kuanza
kufunga mabao, hadi minong’ono ikaanza labda jamaa galasa.
Lakini leo unaposoma makala haya, Didier amekwishaifungia
Yanga mabao 10 katika mechi 17 alizocheza, zikiwemo za kirafiki tatu za
kirafiki.
Amefunga mabao nane kwenye Ligi Kuu, akiwa anamaliza mzunguko
wa kwanza huku anaongoza na amemudu kujihakikishia namba ya kudumu katika
kikosi cha kwanza cha Yanga, mbele ya washambuliaji wengine mahiri kama Said Bahanuzi
na Jerry Tegete.
Didier amewafunika washambuliaji wa kigeni wa timu nyingine
pia, akiwemo Felix Mumba Sunzu Jr. kutoka Zambia, ambaye kwa sasa ndiye
mchezaji ghali zaidi Tanzania akiwa analipwa Sh. Milioni 5 kwa mwezi.
Akiwa katika mwaka wa kwanza wa mkataba wake wa miaka miwili,
dhahiri Kavumbangu sasa amewafanya viongozi wa Yanga wamtazame kwa jicho la
tatu, kwani hiyo tayari ni lulu kwao. Kuna habari pia, ofa zimeanza kumiminika
Jangwani, zikiwemo za klabu za Ulaya kwa ajili ya mchezaji huyo.
Pamoja na hayo, Kavumbangu, mshambuliaji mrefu, mwenye uwezo
wa kumiliki mpira, kasi, nguvu, mbinu na maarifa, bado anahitaji muda kidogo
japo kumalizia mzunguko wa pili Tanzania, ili kututhibitishia zaidi uwezo wake.
Ila kwa sasa hakuna shaka kabisa kusema, amewafunika washambuliaji wote wa
kigeni Tanzania akiwemo Sunzu, mchezaji ghali Tanzania.
Add caption |