Kikosi cha Zanzibar Heroes |
Na Ally Mohamed, Zanzibar
KAMATI ua Utendaji ya Chama cha Soka Zanzibar, (ZFA) imemteua
Salum Bausi kuwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya Zanzibar, Zanzibar Heroes
ambayo itashiriki michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika Mashariki na Kati, CECAFA
Tusker Challenge, baadaye mwezi huu mjini Kampala, Uganda.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mchana katika hoteli
ya Zanzibar Ocean View, iliyopo Kilimani mjini Unguja, ambayo inamilikiwa na ZFA,
Katibu Mkuu wa ZFA, Kassim Hajji Salum, amesema uteuzi huo umefikiwa kulingana
na sifa alizonazo Salum Baus.
Alisema pamoja sifa zake Baus, lakini pia amependekezwa na idadi
kubwa ya Wajumbe wa Kamati Utendaji ya ZFA katika kikao chake cha kuteua kocha
wa timu hiyo.
Hatua ya uteuzi wa kocha huyo imekuja baada ya wadau wa soka
visiwani Zanzibar kuhoji kuchelewa kuteuliwa kocha wa timu ya taifa ya
Zanzibar, huku ikikabiliwa na michuano migumu ya Challenge hivi karibuni.
Salum Bausi anatarajiwa kutangaza kikosi cha timu ya taifa ya
Zanzibar kesho mchana, huku timu hiyo ikitaraijwa kuanza mazoezi Jumanne ijayo,
kujiandaa na michuano ya Kombe la Challenge inayoshirikisha nchi wanachama wa
Baraza la Vyama vya Soka Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), ambayo itaanza
Novemba 24 hadi Desemba 9, mwaka huu.
Msimu uliopita kocha wa Zanzibar katika Challenge alikuwa Muingereza Stewart Hall, ambaye kwa sasa anafundisha Azam FC na baadaye Msaidizi wake, Ahmed Morocco akachukua mikoba yake.
Kwa sasa Morocco ni kocha wa klabu ya Coastal Union ya Tanga inayoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.