Ally Mustafa 'Barthez' |
Na Mahmoud Zubeiry
WASIWASI
kwamba Ally Mustafa ‘Barthez’ akibaki bila kipa mshindani ndani ya Yanga
atabweteka, ndio umemnusuru kipa Mghana, Yaw Berko kutemwa Yanga.
Habari
ambazo BIN ZUBEIRY imezipata kutoka ndani ya Yanga, zimesema kwamba,
Yanga ilifikiria kumtema Berko, lakini kwa uzoefu wao juu ya tabia za wachezaji
wa Kitanzania, wameamua kuachana na wazo hilo.
“Unaweza
kusema umuache Berko, halafu yule Barthez akijiona yuko peke yake, akaanza
kutuzingua, Berko mwenyewe amebadilika mno hivi sasa na yuko tayari kucheza
wakati wowote,”alisema kiongozi mmoja ‘mzito’ wa Yanga.
Berko ambaye
mkataba wake unamalizika Mei mwakani, ataendelea kuitumikia klabu hiyo hadi
mwisho wa mkataba huo na akifanya vizuri ataongezewa mkataba mwishoni mwa msimu.
Kipa huyo
anayelipwa mshahara wa Sh. Milioni 1.5 kwa mwezi, amerudishwa benchi siku za
karibuni baada ya kufululiza kufungwa mabao rahisi, jambo ambalo lilimkera
kocha Mholanzi, Ernie Brandts.
Kwa sababu
hiyo, vyombo vya habari vikaanza kubashiri kwamba ataachwa mwezi ujao kwa
sababu pia, tayari klabu hiyo imesajili mchezaji mwingine wa kigeni, Kabange
Twite kutoka APR ya Rwanda.
Kanuni za
Usajili za Ligi Kuu zinataka wachezaji watano tu wa kigeni kwa kila klabu, na
Yanga tayari inao Yaw Berko, Mbuyu Twite, Haruna Niyonzima kutoka Rwanda,
Hamisi Kiiza kutoka Uganda na Didier Kavumbangu kutoka Burundi.
Lakini
habari zaidi zinasema Kabange atachukua nafasi moja kati ya mbili
zinazotarajiwa kuachwa na wachezaji wawili wa klabu hiyo, ambao watauzwa hivi
karibuni, Niyonzima na Kavumbangu.