Bahanuzi |
Na Mahmoud Zubeiry
WACHEZAJI
wawili wa Yanga, beki Nadir Haroub Ally ‘Cannavaro’ na mshambuliaji Said Rashid
Bahanuzi waliotarajiwa kuondoka leo saa 10:00 jioni kwa ndege ya Qatar Airways
kwenda China, kufanya majaribio ya kucheza soka ya kulipwa, wamezuiwa na klabua
yao hiyo.
Mwenyekiti wa
Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Ahmad Bin Kleb ameiambia BIN
ZUBEIRY mida hii kwamba, sababu za kuzuiwa kwa wachezaji hao ni
kutokana na klabu inayowataka kutofuata taratibu.
“Hawajatuma
barua, hawa wanataka kwenda kienyeji tu, na sisi si kama tumewazuia, tumeitaka
kwanza hiyo klabu ifuate taratibu kwa kutuma barua huku na kujitambulisha, ili
hata hao wachezaji wakipata matatizo tujue tunaanzia wapi,”alisema Bin aKleb.
Mapema leo, Cannavaro,
Nahodha Msaidizi wa Yanga aliiambia BIN ZUBEIRY kwamba wanakwenda China
kwa wiki mbili na baada ya majaribio kama wakifuzu, klabu inayowataka itafanya
mazungumzo na klabu yao.
“Sisi wote
tuna mikataba na klabu, hivyo tukifuzu jamaa itabidi watuhamishe
Yanga,”alisema beki huyo kati
aliyezaliwa Februari 10, mwaka 1982.
Cannavaro
yupo Yanga tangu mwaka 2006, aliposajiliwa kutoka Malindi ya Zanzibar wakati
Bahanuzi amesajiliwa msimu huu akitokea Mtibwa Sugar ya Morogoro.
Mwaka 2009,
Cannavaro alichukuliwa kwa mkopo na klabu ya Vancouver Whitecaps ya Canada na
baada ya miezi sita alirejeshwa Yanga alikoendelea kucheza hadi leo anakwenda
kujaribu bahati yake China.
Bahanuzi
ameingia na zali la aina yake Yanga SC, kwani katika mashindano ya kwanza
kuichezea klabu hiyo alifanikiwa kuibuka mfungaji bora wa Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na kati, Kombe la Kagame.
Hadi sasa, Said
Bahanuzi maarufu kama Spider Man,
ameifungia Yanga mabao 12 katika mechi 14, yakiwemo matatau ya penalti tangu
ajiunge na timu hiyo Julai mwaka huu.
Kwa sasa China ni nchi ambayo mastaa wengi waliokuwa Ulaya
wanakwenda kumalizia soka yao, mfano washambuliaji wawili wa zamani wa Cheslea,
Didier Drogba na Nicolas Anelka waliopo Shenghua Shanghai. Anelka ni kocha
mchezaji.