Na Princess Asia
HATIMAYE
wagombea 23 wamepitishwa kuwania uongozi
katika Uchaguzi wa Chama cha Soka Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), unaotarajiwa
kufanyika Desemba 12, mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi ya DRFA, Juma
Simba, alisema majina hayo yamepitishwa baada ya kufanyika usaili pamoja na
kujadili pingamizi na rufaa zilizowasilishwa.
Alisema
awali wagombea 36 walijitokeza na kuomba nafasi mbalimbali, kabla ya wengine
kuenguliwa ama kujitoa katika kinyang’anyiro kwa sababu mbalimbali.
Aliwataja
waliopitishwa kuwania nafasi ya uenyekiti ni pamoja na Ayoub Nyenzi, Evans Aveva, Brown Ernest na
Almasi Kasongo, huku nafasi ya Makamu Mwenyekiti itawaniwa na Meba Ramadhan,
Salum Mwaking'inda, Gungurungwa Tambaza na Ally Mayai.
Kwa upande
wa nafasi ya Katibu watakaochuana ni pamoja na
Msanifu Kondo na Khamis Ambari, huku waliopitishwa kuwania nafasi ya mjumbe wa mkutano mkuu wa
Shirikisho la soka Tanzania ni Shafii Dauda, Muhsin Balhabouh na Shufaa Jumanne
“Wanaowania ujumbe wa kamati ya utendaji ni
Shaban Kupasya, Siza Chenja, Sunday Mwanahewa, Hamis Kisiwa, Franck Mchaki na
Baraka Mapande wakati watakaowania ujumbe kuwakilisha klabu ni Benny Kisaka,
Juma Pinto, Frank Mchaki na Philemon Ntahilaja”, alisema
Aidha, Simba
aliwataja wajumbe ambao wamechujwa ni Salum Mkemi na Juma Jabir (Uenyekiti),
Issac Mazwile (Makamu Mwenyekiti), Said Tully na Kassim Mustaffa (Katibu Mkuu),
Isaack Mazwile (Mjumbe Mkutano Mkuu TFF) na Chano Karaha (Mjumbe Kamati ya
Utendaji).