Alhaj Manji, Mwenyekiti wa Yanga |
Na Prince Akbar
MAMBO
yameiva Yanga- matumaini ya wapenzi wa klabu hiyo kushuhudia klabu yao ikiwa na
Uwanja mpya wa kisasa yameanza kuonyesha dalili za kutimia, kufuatia uongozi wa
klabu hiyo kusaini makubaliano ya awali na Kampuni ya Beijing Construction
Engineering Group iliyojenga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa ajili ya ujenzi
wa Uwanja wa Kaunda.
Mwenyekiti
wa mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, Alhaj Yussuf Mehboob Manji leo
amesaini makubaliano na Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo, David Zhang, makao makuu
ya klabu hiyo, makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga, Dar es Salaam.
Katika makubaliano
hayo, ujenzi huo wa Uwanja utakaokuwa na uwezo wa kuchukua mashabiki 30,000
hadi 40,000 utaanza rasmi Juni mwakani.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari wakati wa kusaini makubaliano hayo leo mchana, Alhaj Manji
alisema kwamba wanfurahi kuanza safari ya ujenzi wa Uwanja wao na anaamini huo
ni mwanzo wa mzuri wa mipango yao ya kuifanya Yanga ijitegemee kiuchumi.
Katika hatua
nyingine, Manji amesema kwamba katika mipango yao ya kuifanya Yanga ijimudu
kiuchumi, wanafikiria kulikarabati pia jengo dogo la klabu hiyo, liliopo Mtaa
wa Mafia.
Alhaj Manji
alisema Jumatatu kampuni hiyo ya ujenzi kutoka China, ambayo ndiyo iliyojenga
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itachukua vipimo kwenye Uwanja wa Kaunda na
Uongozi wa Yanga kuliwasilisha suala la ujenzi huo kwenye Mkutano Mkuu wa
Wanachama wa klabu hiyo, Desemba 8, mwaka huu.
Alisema
baadhi ya fedha kwa ajili ya uwanja huo wa kisasa watakapo benki na gharama
nyingine zitatokana na michango ya wanachama baada ya kuwa wamepata gharama
nzima za ujenzi za uwanja huo.
Meneja Mkuu
wa Kampuni ya Beijing Cobnstruction Engineering Group alisema wanafurahia
kufikia makubaliano ya awali ya ujenzi wa uwanja na klabu ya Yanga.
Alisema wao
ndio walijenga Uwanja wa Taifa na viwango vya ujenzi vya uwanja huo vilisifiwa
na timu ya taifa ya Brazil iliyokuja kucheza mechi ya kirafiki na Tanzania
mwaka 2010 ikiwa njiani kuelekea Afrika Kusini ambako fainali za kombe la Dunia
zilifanyika.