KUNA wimbo mmoja wa Lady Jaydee unaitwa Siku Hazigandi na kwa wimbo huu pamoja na nyingine za mwanamuziki
huyo wa kihistoria kuwahi kutokea nchini, daima nitaendelea kuwa mpenzi wa
nyimbo zake.
Na Mahmoud Bin Zubeiry |
Wimbo huu una maana pana sana- zaidi ya mtu yeyote
anavyofikiria. Kama utatoa ahadi leo, kwamba mwakani utafanya kitu fulani hata
kama hauna dhamira, tarajia hiyo siku itafika na ukweli au uongo wako
utajulikana siku hiyo.
Mimi wimbo huu huwa unanifariji sana kwamba, kama unakabiliwa
na matatizo, mitihani ya dunia, usikate tamaa, siku hazigandi, ipo siku, siku
za mashaka zitaisha na Mungu atakujaalia furaha tena.
Kama unadharau watu kwa majaaliwa yako, basi fahamu siku
hazigandi, ipo siku, siku zako za utawala zitakwisha nawe utaonja machungu ya
dunia. Lady Jaydee aliimba.
Juzi, Mwenyekiti wa Yanga, Alhaj Yussuf Mehboob Manji alisaini
makubaliano ya awali na Kampuni ya Beijing Constructions Engineering Group
iliyojenga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa
Kaunda, unaomilikiwa na klabu hiyo.
Manji alisaini makubaliano hayo na Meneja Mkuu wa Kampuni
hiyo, David Zhang, mbele ya Waandishi wa Habari, makao makuu ya klabu hiyo,
makutano ya mitaa ya Jangwani na Twiga, Dar es Salaam.
Katika makubaliano hayo, ujenzi huo wa Uwanja utakaokuwa na
uwezo wa kuchukua mashabiki 30,000 hadi 40,000 utaanza rasmi Juni mwakani.
Akizungumza na Waandishi wa Habari wakati wa kusaini
makubaliano hayo juzi mchana, Alhaj Manji alisema kwamba wanafurahi kuanza
safari ya ujenzi wa Uwanja wao na anaamini huo ni mwanzo wa mzuri wa mipango
yao ya kuifanya Yanga ijitegemee kiuchumi.
Katika hatua nyingine, Manji alisema kwamba katika mipango
yao ya kuifanya Yanga ijimudu kiuchumi, wanafikiria kulikarabati pia jengo dogo
la klabu hiyo, liliopo Mtaa wa Mafia.
Alhaj Manji alisema kesho kampuni hiyo ya ujenzi kutoka
China, ambayo ndiyo iliyojenga Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam itachukua vipimo
kwenye Uwanja wa Kaunda na Uongozi wa Yanga kuliwasilisha suala la ujenzi huo kwenye
Mkutano Mkuu wa Wanachama wa klabu hiyo, Desemba 8, mwaka huu.
Alisema baadhi ya fedha kwa ajili ya uwanja huo wa kisasa
watakapo benki na gharama nyingine zitatokana na michango ya wanachama baada ya
kuwa wamepata gharama nzima za ujenzi za uwanja huo.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Kampuni ya Beijing Constructions
Engineering Group alisema wanafurahia kufikia makubaliano ya awali ya ujenzi wa
uwanja na klabu ya Yanga.
Alisema wao ndio walijenga Uwanja wa Taifa na viwango vya
ujenzi vya uwanja huo vilisifiwa na timu ya taifa ya Brazil iliyokuja kucheza
mechi ya kirafiki na Tanzania mwaka 2010 ikiwa njiani kuelekea Afrika Kusini
ambako fainali za kombe la Dunia zilifanyika.
Wakati naihariri habari kuhusu makubaliano hayo, nilikumbuka
tukio la Mwenyekiti wa Simba, Alhaj Ismail Aden Rage kusaini mkataba na
Waturuki kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja wa kisasa wa klabu yake.
Leo ni zaidi ya mwaka sasa tangu Rage asaini makubaliano
hayo, lakini habari iliyopo, hata hicho kiwanja kwa ajili ya kuujenga Uwanja huo,
bado hawajakamilisha malipo yake.
Maana yake nini? Ilikuwa ni kuwahadaa wanachama wa Simba au?
Atajua mwenyewe Rage, lakini kwa vyovyote leo anaumbuka mwenyewe kwa sababu
siku zimepita, hazikuganda na wana Simba bado hawana ndoto za kuwa na Uwanja
wao chini ya Mwenyekiti huyo mwenye asili ya Kisomali.
Nilicheka sana ‘juzi juzi’ alipoibuka na ahadi ya kuipeleka
timu Ulaya kabla ya kuanza kwa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu na Ligi ya Mabingwa
Afrika mwakani. Nikasema, haya shauri yake, hajajua tu siku hazigandi!
Tuachane na ya Rage, huyu tumekwishamzoea mzee wetu. Hiyo
ndio starehe yake na bila shaka hata yeye mwenyewe anajijua kama watu wanamjua
desturi yake, sema mkavu tu babu huyu!
Manji si Mwenyekiti wa kwanza wa Yanga kutoa ahadi ya kujenga
Uwanja wa Kaunda na wakati kesho mkandarasi anakwenda kufanya vipimo, nataka
niwakumbushe tu wasomaji wangu, wakati Tarimba Abbas, Francis Kifukwe wakiwa
viongozi wakuu wa klabu hiyo, walikwenda wakandarasi kupima Jangwani.
Huo ni wakati ambao haijafikiriwa kama iko siku itatokea timu
inaitwa Azam FC na leo klabu hiyo ina miaka sita, lakini Uwanja wa Kaunda upo
kama alivyouacha marehemu Tarbu Mangara, tena umezidi kuchakaa kwa kukosa japo
matunzo tu.
Azam FC leo ina Uwanja wa maana na akademi, ambayo hadi
Mwanasoka Bora wa zamani Afrika, Abedi Ayew Pele alipozuru nchini aliusifia.
Nina kila sababu ya kumuamini Manji, kwa sababu kila
ukiitazama Yanga ya leo, bila ya yeye sijui ingekuwaje.
Manji aliingia Yanga mwaka 2006 baada ya jitihada
zilizofanywa na wanachama wa klabu hiyo akina Theonist Rutashoborwa (sasa
marehemu), Mzee wa Mpunga, Mawakili Lugaziya na Matunda na baadhi ya Waandishi
wa Habari za michezo wenye mapenzi na klabu hiyo, kuanzisha harambee ya Saidia
Yanga, kufuatia hali mbaya ya kiuchumi kukithiri ndani ya klabu hiyo, chini ya
uongozi wa Francis Kifukwe.
Katika kutafuta misaada ya kuibeba timu wakati huo ipo kwenye
michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, maarufu kama Kombe la Kagame
ndipo wakampata Manji naye kwa mapenzi yake, akasema; “Nitaubeba mzigo wote”,
na kweli hadi leo, amekuwa akiilea Yanga tangu kama mfadhili hadi sasa
Mwenyekiti.
Hadi sasa, Manji ameingia kwenye historia Yanga kama miongoni
mwa watu muhimu kuwahi kutokea kwenye klabu hiyo, bila hata ya ahadi ya Uwanja.
Naandika makala haya kwa sababu kwa uzoefu wangu, Manji ana
desturi ya kususa anapopata upinzani kidogo kutoka kwa watu wenye mlengo
tofauti naye.
Amewahi kususa zaidi ya mara mbili na kuifanya Yanga iyumbe
kidogo- wakati Wakili Imani Madega na Lloyd Nchunga wakiwa viongozi wa Yanga.
Na Manji atarajie akiwa Mwenyekiti wa Yanga, lazima
ataendelea kukabiliana na upinzani kwani hiyo ndiyo demokrasia katika vitu
ambavyo vinagusa hisia za wengi.
Hivyo basi, hata wazo lake la ujenzi wa Uwanja, si ajabu
wakatokea ‘maputo’ washajazwa upepo wakaanza kulipinga na kumzulia Mwenyekiti
wao mambo.
Manji ajiandae kwa lolote, ili mradi tu ahakikishe anatimiza
ahadi ambayo kwa sasa baadhi ya wana Yanga wanalala macho wakiomba Juni 2013
ifike kijiko kishuke Jangwani kuchimba.
Tofauti na kutimiza ahadi hiyo, hakika Manji atajishushia
heshima yake kwa kiasi kikubwa mbele ya wana Yanga na jamii ya Watanzania kwa
ujumla.
Na mashabiki ni watu ‘hawana adabu’, wanaweza kuthubutu hata
kumfananisha na Rage. Hivyo basi, Manji ajue kwamba, ahadi ya ujenzi wa Uwanja
wa Kaunda, imebeba mustakabali wa heshima yake.
Wasalam!