King Pele |
Na Mahmoud Zubeiry
MWANASOKA bora
wa zamani Afrika, Abedi Ayew Pele ambaye pia ni Balozi wa Shirikisho la Soka la
Kimataifa (FIFA), amesema kwamba katika mechi ya jana ya Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara kati ya Yanga na Azam alivutiwa na soka, ushindani, kiwango na
uwezo wa wachezaji, ingawa amemtaja Haruna Hakizimana Fadhil Niyonzima kuwa
ndiye aliyemvutia zaidi.
Pele alisema
wachezaji wengi waliocheza jana wana viwango vya kucheza Ulaya, ingawa
amemsifia zaidi Niyonzima, kwamba anastahili kabisa kucheza moja ya klabu kubwa
hata Ulaya.
“Aliyevaa
jezi namba nane wa Yanga, anajua sana. Niliambiwa ni Mnyarwanda, Yule kijana
mzuri sana, ni mtaalamu,”alisema Pele akizungumza na Waandishi wa Habari mchana
wa leo katika ziara yake makao makuu ya klabu ya Azam, Azam Complex, Chamazi,
Dar es Salaam.
Pele ambaye
akiwa Chamazi amejionea mambo mbalimbali, ikiwemo mradi wa maendeleo ya soka ya
vijana, Academy aliousifia sana na kusema utaleta matunda makubwa Tanzania
baadaye, alikuwepo Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam jana Yanga ikiilaza Azam 2-0.
Akiizungumzia
Azam kwa ujumla, amesema miaka kadhaa ijayo itakuwa klabu kubwa yenye hadhi
sawa na Manchester United ya England kutokana na uwekezaji wake mzuri.
Alisema akademi
ya Azam ni nzuri na bora kuliko hata akademi yake. “Kwetu tuna akademi nyingi,
lakini nyingi ni za wawekezaji wa nje (klabu za Ulaya), lakini hii ni ya Azam,
safi sana. Akademi yangu ni ndogo tu, haiifikii hii kwa ubora, nami nina ndoto
za kufanya kitu kama hiki, nadhani nitajifunza mengi kutoka kwa Azam,”alisema Pele.
Pele pia aliishauri
Azam kuachana na desturi ya kuchukua wachezaji wa nje ya nchi, kwani kama
wataitumia vizuri akademi yao kwa kusaka vipaji zaidi nchi mzima, mbele ya watu
zaidi ya Milioni 40 watapata wachezaji bora.
“Kama kwa
lengo la kubadilishana tu uzoefu sawa, lakini kama una kademi nzuri kama hii,
kwa nini uchukue mchezaji kutoka Ghana, hii nchi yenu ina watu zaidi ya Milioni
40, mnaweza kutengeneza wachezaji wengi wazuri na nyinyi mkauza Ulaya,”alisema
Pele ambaye ameahidi kuanzisha ushirikiano wa akademi yake na ya Azam, baada ya
kuombwa na Rais wa TFF, Leodegar Tenga.
Akiizungumzia
Ligi Kuu ya Tanzania baada ya kuona mechi ya Yanga na Azam, Pele alisema ina
ubora sawa na ligi nyingine kubwa Afrika na akasema sasa kinachotakiwa ni
kuongeza maboresho.
Kuhusu wachezaji,
kulingana na alivyoona mechi ya jana, Pele alisema kwamba wana uwezo sawa na
wachezaji wengi duniani na ili watimize ndoto za kucheza Ulaya, wanatakiwa kuongeza
juhudi
Awali ya
hapo, mshambuliaji huyo wa zamani wa kimataifa wa Ghana na klabu ya Olympique
Marseille ya Ufaransa, aliwaambia wachezaji chipukizi wa Tanzania kwamba,
hakuna njia ya mkato katika kutafuta mafanikio na kuwataka kufanya jitihada ili
watimize ndoto zao, ikiwa ni pamoja na Serengeti Boys kuhakikisha inafuzu
kucheza fainali za Afrika mwakani.
Pele, ambaye
aliiongoza Marseille kutwaa ubingwa wa Ulaya mwaka 1992 akifunga moja ya mabao
dhidi ya AC Milan ya Italia, alisema hayo Jana asubuhi wakati alipotembelea
Kiti cha ufundi cha Karume kushuhudia programu ya mazoezi ya vijana wadogo
inayofanyika kila misho wa wiki kwenye Uwanja wa Karume ambako watoto wa
kuanzia umri wa miaka sita hadi 17 hufundishwa mbinu za kusakata soka.
"Katika
kufikia mafanikio hakuna njia ya mkato," alisema Pele ambaye ameletwa
nchini na Shirikisho la Kimataifa la Vyama vya Mpira wa Miguu (FIFA) kuangalia
shughuli mbalimbali za maendeleo ya mpira wa miguu nchini.
"Tunaona
wachezaji wenye vipaji vikubwa duniani wakifanya jitihada kubwa ili waweze
kucheza kwa kiwango cha juu. Bila ya kufanya juhudi, kujituma na kudhamiria
huwezi kufanikiwa.
Niyonzima kushoto akimiliki mpira katika mechi ya jana. Kulia ni Erasto Nyoni |
"Wale
wenye vipaji vikubwa, lakini hawafanyi jitihada watabakia I. Wale wasiojaliwa
kuwa na vipaji, lakini wanafanya jitihada, watakwenda mbele na kupata
mafanikio," alisema nyota huyo ww Ghana ambaye alijijengea jina kwa
kufunga mabao safi na muhimu kwa nchi yake na klabu ya Olympique Marseille
wakati ikitamba katika soka barani Ulaya.
"Soka
barani Afrika Lina mazingira yanayofanana. Hakuna motto wa waziri anayecheza
soka. Wala hakuna mtoto wa mwanasheria au mfanyakazi ww benki ambaye anacheza
soka. Soka inachezwa na watu wanaotoka kwenye familia ambazo hazina maisha
mazuri na hivyo man nafasi sawa na wengine wote. Mnachotakiwa kufanya ni kujituma,
kudhamiria na kufanya jitihada ili mfungue mlango wa mafanikio.
Pele, ambaye
watoto wake wainaichezea Marseille, pia aliwataka wachezaji wa timu ya Taifa ya
Vijana walio na umri china ya miaka 17 kufanya kila wawezalo ili wafuzu kucheza
fainali za Mataifa ya Afrika zitakazofanyika Algeria mapema mwakani.
"Mkifuzu
mtakuwa mmefungua milango ya mafanikio ya maisha yenu," alisema gwiji huyo
ambaye anaiwakilisha FIFA katika kufuatilia programu mbalimbali za maendeleo.
"nikiwaangalia naona mna man uwezo wa kuwaondoa wapinzani wenu na
nitafuatilia mechi yenu. Mkifuzu tutakuwa wote na nitawaunga mkono.
Pele, ambaye
kwa sasa anamiliki shule ya mpira wa miguu ambayo imeshanikiwa kutwaa Kombe la
FA mara moja, ameambatana na Mkurugenzi wa Maendeleo wa FIFA kwa nchini za
Kusini mwa Afrika, Ashford Mamelodi na mmoja wa viongozi wa Idara ya Mawasiano
ya FIFA, Emmanuel, atakuwa nchini kwa siku tatu ambazo atazitumia kupata
taarifa za shughuli mbalimbali za maendeleo, zikiwemo za soka la watoto
(grassroots), soka la vijana, soka la wanawake na miradi mingine ya maendeleo.