Zen C; Atatoka kwenye pingamizi nne? |
Na Princess Asia
MWANDISHI wa Habari Mwandamizi wa magazeti ya serikali, Daily
News, Habari Leo na Spoti leo, Zena Chande ‘Zen C’, ni miongoni mwa wagombea
sita wa nafasi mbalimbali za uongozi katika Chama cha Soka kwa Wanawake
Tanzania (TWFA) waliowekewa pingamizi na wadau wa mchezo huo.
Ofisa Habari wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Boniphace
Wambura Mgoyo ameiambia BIN ZUBEIRY ‘mida hii’ kwamba, Kwa
mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya TWFA, Ombeni Zavala, wagombea wengine
ni Joan Minja anayewania nafasi ya Mwenyekiti ambaye amewekwa pingamizi na
wadau sita na Isabellah Kapera ambaye anagombea Uenyekiti amewekewa pingamizi
moja.
Wagombea watatu wa nafasi ya Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa TFF
nao wamewekewa pingamizi akiwemo Zen C, aliyewekewa pingamizi nne, wengine ni Julliet
Mndeme (pingamizi sita), na Jasmin Soud mwenye pingamizi tatu, wakati Rahim
Maguza anayewania ujumbe wa Kamati ya Utendaji amewekewa pingamizi moja.
Wambura amesema pamoja na pingamizi hizo, wagombea wote
wanatakiwa kuhudhuria usaili wakiwa na vyeti vyao halisi vya kitaaluma
utakaofanyika Oktoba 12, 13 na 14 mwaka huu kwenye ofisi za TFF zilizopo Uwanja
wa Karume, Dar es Salaam kuanzia saa 3:00 asubuhi.