Bahanuzi |
Na Mahmoud Zubeiry
BEKI Kevin Yondan na mshambuliaji Said Bahanuzi waliokuwa nje
ya Uwanja kwa zaidi ya wiki mbili kutokana na kusumbuliwa na majeruhi, leo
wanatarajiwa kuanza programu rasmi ya mazoezi na wenzao baada ya kupata ahueni
ya kutosha.
Wachezaji hao wamekuwa wakifanya mazoezi mepesi kwa zaidi ya
wiki moja baada ya kupata ahueni kidogo na sasa wamepona kabisa na leo kocha
Mholanzi, Ernie Brandts anatarajiwa kuwajumuisha kwenye programu yake kamili,
Uwanja wa sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
Yanga imerejea kutoka Arusha, ambako Jumamosi ilivuna pointi
tatu kwa ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji JKT Oljoro, Uwanja wa Sheikh Amri
Abeid na kupanda nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara, wakitimiza pointi 20 baada ya kucheza mechi 10.
Yanga sasa iko nyuma kabisa ya wapinzani wao wa jadi, Simba
SC wanaoongoza Ligi Kuu kwa pointi zao 22, baada ya kucheza mechi 10 pia.
Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame
sasa wanajiandaa na mchezo wao ujao wa ligi hiyo, dhidi ya Mgambo JKT Jumatano
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mgambo JKT pamoja na kwamba imepanda Ligi Kuu msimu huu,
lakini imeonyesha ni timu ya ushindani baada ya kutoa sare ya bila kufungana na
Simba SC, Uwanja wa Mkwakwani, Tanga.
Kwa sababu hiyo, Yanga wamechukua tahadhari ya kutosha kuelekea
mchezo huo na tangu jana Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah Ahmad
Bin Kleb amekuwa ‘akienda mbio’ kuhakikisha timu inashinda keshokutwa.
Kurejea kwa Yondan na Bahanuzi kunaongeza matumaini ya
ushindi kwa Yanga katika mchezo huo, ingawa upande mwingine ni mtihani kwa
Brandts, kwani katika kipindi ambacho wachezaji hao wako ‘wadini’, walioshika
nafasi zao wamekuwa wakifanya vizuri.
Mbuyu Twitwe aliyehamishwa kutoka beki ya kulia hadi beki ya
kati tangu Yondan aumie Oktoba 3, amekuwa akifanya vizuri sawa na Jerry Tegete
aliyempokea Bahanuzi Oktoba 8, alipoumia naye amekuwa akifanya vizuri pia.
Kwa kuzingatia Twite alikuwa ‘uchochoro’ alipokuwa akicheza
pembeni, watu wanasubiri kuona kama Brandts atamrudisha huko huko baada ya Yondan
kurejea, au ataamua mmoja kati yao na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ataanzia benchi.
Upande wa Tegete na Bahanuzi, kuna uwezekano mmoja wao
atakuwa anaanzia benchi kwa sasa na mwingine kumpokea mwenzake baadaye.