Yondan |
Na Mahmoud Zubeiry
BEKI Kevin
Yondan na mshambuliaji Said Bahanuzi wataendelea kuwa nje ya Uwanja kesho,
wakati timu yao, Yanga SC itakapokuwa ikiwania pointi tatu katika mfululizo wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kutokana na hali zao kutoimarika na habari
mbaya zaidi ni kwamba, beki Job Ibrahim naye hatashiriki mechi ya kesho.
Job, ambaye
amekuwa beki wa akiba tangu mwanzoni mwa msimu, aliumia kifundo cha mguu mazoezini
juzi na jana hakufanya mazoezi kabisa, wakati Yondan na Bahanuzi wanaendelea na
programu ya mazoezi mepesi na hadi jana hakuna mmoja kati yao aliyekuwa tayari
kuanza programu kamili ya mazoezi ya kocha Mholanzi, Ernie Brandts.
Maana yake,
Mbuyu Twite ataendelea kucheza pamoja na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika beki
ya kati, wakati Jerry Tegete ataendelea kucheza na Didier Kavumbangu katika
safu ya ushambuliaji.
‘Dogo’ Simon
Msuva amemaliza adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa Oktoba 3, mwaka huu katika
mechi dhidi ya Simba na ilikuwa aanze kucheza tangu Jumamosi, ila kutokana na
kiwango duni cha Hamisi Kiiza alichoonyesha kwenye mechi na Ruvu Shooting
Jumamosi, kesho kinda huyo anaweza kurudishwa uwanjani.
Kiiza aliichezea
Yanga kwa mara ya kwanza siku hiyo akitokea benchi kipindi cha pili, tangu
atolewe kipindi cha kwanza katika mechi dhidi ya Simba, Oktoba 3, mwaka huu.
Kiiza alikuwa
kwao, Uganda, alipokwenda kuichezea timu yake ya taifa, The Cranes
katika mchezo wa marudiano wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la
Mataifa ya Afrika mwakani nchini Afrika Kusini.
Uganda ilitolewa na Zambia kwa mikwaju ya penalti baada ya
sare ya jumla ya 1-1, Zambia wakianza kushinda nyumbani 1-0 na Uganda wakashinda
kwao 1-0 pia mwishoni mwa wiki, hivyo mchezo kuhamia kwenye mikwaju ya penalti,
ambako timu ya Kiiza ilitolewa.
Yanga imeweka kambi katika hoteli ya Uplands, Changanyikeni,
Dar es Salaam huku ikiendelea kufanya mazoezi kwenye Uwanja wa shule ya sekondari
ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
Yondan aliyeumizwa na kiungo wa Simba, Haruna Moshi ‘Boban’
katika mechi baina ya wapinzani hao wa jadi, Oktoba 3, mwaka huu, wakati Bahanuzi ‘Spider Man’ alichanika
nyama za paja la mguu wa kulia katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba Oktoba 8, mwaka huu.
Bahanuzi
aliumia dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar
na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete
katika mechi ambayo Yanga ililala 1-0, beo pekee la Themi Felix.
Bahanuzi
ndiye tegemeo la mabao la Yanga kwa sasa, kwani tangu ajiunge na timu hiyo
akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, ameifungia mabao 12 katika mechi 13, ikiwemo
ile dhidi ya Kagera aliyocheza kwa dakika 23 kabla ya kuumia na kutoka.
Yanga kwa
sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 14,
baada ya kucheza nane, kushinda nne, sare mbili na kufungwa mbili.
Simba
iliyocheza mechi tisa, inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 19, ikifuatiwa na
Azam FC yenye pointi 17, iliyocheza mechi saba.