Kavumbangu; Mfungaji wa bao la kwanza la Yanga (Picha na Maktaba ya BIN ZUBEIRY) |
Na Prince Akbar, Mwanza
YANGA SC leo imezinduka baada ya kupata ushindi wa mabao 3-1
katika mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya wenyeji Toto
African, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza.
Matokeo haya, yanaifanya Yanga itimize pointi 11, katika
mechi saba ilizocheza hadi sasa, ikiwa imefungwa mbili, sare mbili na kushinda tatu,
inazidiwa pointi tano na wapinzani wake wa jadi, Simba SC wanaoongoza ligi hiyo
kwa pointi zao 16, wakifuatiwa na Azam wenye pointi 13.
Hadi mapumziko, Yanga walikuwa tayari mbele kwa mabao 2-0, yaliyopachikwa
kimiani na mshambuliaji wa kimataifa wa Burundi, Didier Kavumbangu na beki wa
kimataifa wa Rwanda, mwenye asili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC),
Mbuyu Twite.
Kavumbangu alifunga bao la kwanza dakika ya pili, baada ya
kuuwahi mpira uliotemwa na kipa Erick Ngwengwe kufuatia kona iliyochongwa na
Haruna Niyonzima, hilo likiwa bao lake la tano ndani ya mechi 11 tangu ajiunge
na Yanga msimu huu akitokea Atletico ya kwao, Burundi.
Baada ya bao hilo, Yanga waliendelea kulisakama lango la Toto
na dakika ya 21, Mbuyu Twite akaunganisha kona ya chini chini iliyochongwa na
Niyonzima.
Toto ilipoteza nafasi nzuri ya kufunga dakika ya 42, baada ya
kupata penalti, kufuatia beki mmoja wa Yanga kuunawa mpira kwenye eneo la
hatari, baada ya Wana Kishamapanda kufanya shambulizi kali la kushitukiza,
lakini kiungo Emanuel Swita akapiga nje.
Swita alipiga penalti nzuri tu ya chini pembeni kabisa,
lakini vipimo vyake vikazidi kidogo, mpira ukatoka nje, ingawa Berko aliifuata
vizuri pembeni kabisa kulia kwake na angeweza kuokoa.
Kipindi cha pili Toto waliingia kwa kasi zaidi na kuanza
kulishambulia lango la Yanga mfululizo, wakitawala zaidi sehemu ya kiungo.
Katika dakika ya 54 mshambuliaji Mussa Said aliifungia Toto
bao safi, baada ya kipa Yaw Berko kutoka langoni.
Baada ya bao hilo, Toto walizidi kutawala mchezo na kukosa
mabao mawili ya wazi- hapo ndipo kocha Mholanzi, Ernie Brandts akawatoa viungo
Frank Domayo na Athumani Idii ‘Chuji’ na kuwaingiza Shamte Ally na David Luhende.
Walipoingia Shamte na Luhende wote walienda kushambulia pembeni
na Haruna Niyonzima na Nurdin Bakari wakarudi katikati.
Mabadiliko hayo yaliisaidia Yanga kupata bao la tatu dakika
ya 68, lililofungwa kitaalamu na mshambuliaji Jerry Tegete ambaye alimpiga
chenga kipa Ngwengwe baada ya kupokea pasi ya Oscar Joshua.
Baada ya bao hilo, Kocha wa Toto, Johh Tegete naye alifanya
mabadiliko akiwatoa Mussa Said na Evarist Maganga na kuwaingiza Heri Mohamed na
Heri Kyaruzi. Hata hivyo, pamoja na mabadiliko hayo, Yanga waliendelea kutawala
mchezo hadi filimbi ya mwisho.
Kwa ushindi huu, Yanga imelipa kisasi cha mara ya mwisho timu
hizo, zilipokutana kwenye Uwanja huo, Jumapili ya Aprili 15, mwaka huu, Toto
walipoibuka na ushindi wa mabao 3-2.
Katika mchezo huo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Yaw Berko, Juma
Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Mbuyu Twite, Athumani Iddi ‘Chuji’/Shamte
Ally, Frank Domayo/David Luhende, Haruna Niyonzima, Jerry Tegete, Didier
Kavumbangu na Nurdin Bakari.
Toto; Erick Ngwengwe, Kulwa Greyson, Eric Mulilo, Evarist
Maganga/Heri Kyaruzi, Peter Mabula, Hamisi Msafiri, Emanuel Swita, Haroun
Athumani, Mohamed Hussein, Suleiman Kibuta na Mussa Said/Heri Mohamed.