Msuva kulia akishangilia na wenzake baada ya kufunga bao la kwanza. Kushoto ni Jerry Tegete na David Luhende |
Na Mahmoud Zubeiry
YANGA SC imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, baada ya kuichapa Polisi Morogoro mabao 3-0 kwenye
Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo, unaifanya Yanga itimize pointi 17, baada ya
kucheza mechi tisa na kuendelea kusimama katika nafasi ya tatu, nyuma ya Azam FC
yenye pointi 18, baada ya sare ya 1-1 na Ruvu Shooting Uwanja wa Chamazi, nje
kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Ruvu walipata bao lao kupitia kwa Seif Abdallah na Kipre
Tcheche akaisawazishia Azam.
Uwanja wa Taifa, hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa
mabao 2-0 yaliyotiwa kimiani na washambuliaji Simon Msuva na Didier Kavumbangu.
Msuva alikuwa wa kwanza kuwainua vitini mashabiki wa Yanga
dakika ya tano kabla ya dakika moja baadaye, Mrundi Kavumbangu naye kuwapa raha
mashabiki wa timu hiyo.
Yanga ingekwenda kupumzika ikiwa inaongoza kwa mabao 3-0 kama
mkwaju wa penalti wa Haruna Niyonzima usingegonga mwamba na kurudi uwanjani
kabla ya mabeki wa Polisi kuondosha kwenye hatari.
Refa Alex Mahagi kutoka Mwanza alitoa penalti hiyo, baada ya
Msuva kuangushwa na beki John Bosco kwenye eneo la hatari wakati anakwenda
kufunga.
Kipindi cha pili Yanga walirudi kwa kasi tena na kuendelea
kulishambulia lango la Polisi, ingawa walipoteza nafasi nyingi na kutumia moja
tu, dakika ya 58, mfungaji Hamisi Kiiza aliyeingia kuchukua nafasi ya Jerry Tegete.
Katika mechi nyingine za Ligi Kuu leo, Coastal Union
iliifunga 1-0 African Lyon Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, Mtibwa Sugar
imelazimishwa sare ya 1-1 na Kagera Sugar Uwanja wa Manungu, Morogoro.
Matokeo ya leo yanaziweka karibu mno, Simba, Azam na Yanga pale
juu, kiasi kwamba ushindani na uhondo wa ligi hiyo unaongezeka.
Katika mchezo wa leo, kikosi cha Yanga kilikuwa; Ally Mustafa
‘Barthez’, Shadrack Nsajigwa, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ (Nahodha),
Mbuyu Twite, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Haruna Niyonzima/Nurdin Bakari,
Jerry Tegete/Hamisi Kiiza, Didier Kavumbangu na David Luhende/Nizar Khalfan.
Polisi; Manji Kulwa/Kondo Salum, Nahodha Bakari, John Bosco,
Noel Msakwa, Salmin Kissi, Hamisi Mamiwa, Bantu Admin/Paul John, Paschal Maige,
Mokili Rambo (Nahodha), Malimi Busungu na Nicholas Kabipe/Keneth Masumbuko.
Katika mchezo wa awali wa utangulizi, Yanga B imeifunga TMK
United ya Ligi Daraja la Pili, mabao 6-1 katika mchezo wa utangulizi kabla ya
mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, kati ya Yanga na Polisi Morogoro.
Mabao ya Yanga yamefungwa na Georgeb Banda matatu katika
dakika za 61, 70 na 72, Hussein Moshi dakika ya 12 na Rehani Rehani dakika ya
19 na 27, wakati la kufutia machozi la TMK United, lilifungwa na Abdi Hashimu
dakika ya 62.