ALIYEWAHI kuwa kocha wa Yanga, Mganda
Samuel Timbe aliwahi kusema maneno ambayo yalinikumbusha mbali kidogo. Yalinikumbusha
mwaka 2007, wakati aliyekuwa kocha wa Yanga, Mserbia Milutin Sredojevic ‘Micho’
anaamua kuachana na Yanga, licha ya kuipigisha hatua fulani mbele, kutoka
ilipokuwa.
Na Mahmoud Zubeiry |
Timbe alisemaje? Alisema kufanya kazi Yanga
ni vigumu mno, mashabiki na viongozi wale si waelewa na hawana subira.
Alisema hivyo, baada ya kupata kashikashi
kidogo baada ya mechi ya pili ya Kundi B, michuano ya Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati, Kombe la Kagame mwaka jana, kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam, dhidi ya Elman ya Somalia ambayo ilimalizika kwa timu hiyo kushinda
mabao 2-0, lakini bao la pili likipatikana dakika za lala salama.
Yanga ilikuwa inaongoza 1-0 kwa muda mrefu,
bao ambalo lilitiwa kimiani na Davies Mwape, lakini kwa kuichukulia Elman ni
timu dhaifu, hawakuridhishwa na ‘bao moja tu’, hivyo alipoingia Hamisi Kiiza na
kufunga la pili dakika za lala salama, walidhani angekuwapo uwanjani kwa muda
mrefu angefunga zaidi.
Hiyo ni imani iliyotokana na cheche za
mshambuliaji huyo wa Uganda wakati huo za kufunga mabao akiwa na timu ya taifa
ya vijana chini ya umri wa miaka 23, aliifunga Tanzania mabao matatu katika
mechi mbili na Kenya mabao matatu katika mechi moja.
Kweli, Kiiza alikuwa mkali wa mabao wakati
huo, moto ambao aliingia nao hadi Yanga, lakini bado wana Yanga walipaswa
kuheshimu uamuzi wa kocha, kwa kuwa yeye ndiye aliyekuwa anajua hali halisi kuhusu
wachezaji wake.
Hakuna kocha ambaye anapelekea timu yake
uwanjani ikaadhibiwe, kocha yeyote anaingiza timu uwanjani kusaka ushindi, na
ili atimize malengo hayo, lazima awape nafasi wachezaji hodari.
Lakini hali halisi ya Kiiza siku hiyo ni
kwamba aliwasili Dar es Salaam usiku wa kuamkia mechi akitokea Kenya, ambako
alikuwa akiichezea Uganda dhidi ya wenyeji kuwania tiketi ya Michezo ya Afrika
(AAG) - hakuwahi kufanya mazoezi na Yanga hata siku moja.
Lakini hilo wana Yanga hawakulitambua na
baada ya mchezo wakamghasi kocha, jambo ambalo liliibua tetesi nyingi baadaye,
eti amesusa kufundisha, wakati alikuwa anaumwa.
Hata katika mechi ya tatu na ya mwisho ya
Kundi B dhidi ya Bunamwaya ya Uganda, Timbe aliingia lawamani tena kwa
mabadiliko aliyofanya, kumtoa Nsajigwa Shadrack na kumuingiza Julius Mrope.
Siku hiyo, Timbe alitumia ujanja mmoja,
wingi ya kulia aliweka mabeki watupu, chini Nsajigwa na juu Godfrey Taita, lengo
ni kuwadhibiti Bunamwaya kuanzia kwenye himaya yao katika upande huo, ambao ina
wachezaji hodari sana.
Lakini akiwa tayari amejikwishavuna mabao
mawili, hakuona sababu ya kutopunguza beki na kuingiza winga ili kuongeza kasi
ya mashambulizi katika kusaka mabao zaidi, ndipo akamtoa Nsajigwa, Taita
akarudi nyuma na Mrope akaenda kucheza mbele. Lakini ikatokea bahati mbaya,
kitu ambacho ni kawaida katika soka, mabadiliko hayakuwa na tija na Yanga
ikaruhusu mabao mawili kabla ya Davies Mwape kufunga la ushindi dakika za
majeruhi.
Lakini pia, Nsajigwa tayari alikuwa ana
kadi ya njano, ina maana angefanya faulo nyingine angetolewa nje. Kadhalika,
beki huyo alijiunga na wenzake akitokea kwenye fungate la harusi yake na
alikosa mechi ya kwanza dhidi ya El Merreikh.
Hali iliyotokea, Timbe hakuipenda na makosa
wakati mwingine makocha wote duniani hufanya na vizuri zaidi kwa weledi, kosa
si somo kubwa na ndiyo maana mwisho wa mashindano Yanga ilikuwa bingwa.
Sasa narudia kukumbushia ya Micho kabla
sijaendelea na mada ya leo; mwaka 2007 Micho aliifikisha Yanga hatua ya 16 bora
ya Ligi ya Mabingwa Afrika, hatua ambayo mara ya mwisho klabu hiyo ilifika
mwaka 2001 na kutolewa na Mamelodi Sundown ya Afrika Kusini, ikiwa chini ya
kocha Charles Boniface Mkwasa.
Kwa Micho, timu yake ilitolewa na Esperance
ya Tunisia kwa mabao 3-0, waliyofungwa Tunis na baadaye sare ya bila kufungana
Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza.
Tayari wakati huo kanuni ya timu
zinazotolewa kwenye 16 bora ya Ligi ya Mabingwa zinahamia kwenye Kombe la
Shirikisho ilikwishaanza kutumika na Yanga ikahamia huko, ilipotolewa na El
Merreikh ya Sudan kwa mabao 2-0 ya ugenini, wakianza na sare ya bila kufungana
mjini Mwanza.
Yanga iliweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza
kufika hatua hiyo kabla ya Simba nao kufika huko mwaka jana. Mbali na
kuifikisha mbali kwenye michuano ya Afrika, Micho pia aliifikisha Yanga fainali
ya ligi ndogo ambako ilifungwa na Simba kwa penalti, langoni mwa Wekundu wa
Msimbazi akiwa amesimama Kaseja Juma na kuokoa penalti muhimu za akina Abdi
Kassim na Abuu Mtiro.
Hakika ulikuwa mwanzo mzuri kwa kocha Micho
na ilitarajiwa msimu uliofuata angeiboresha timu, hususan katika safu ya
ushambuliaji ili ifanye vizuri zaidi, lakini ikawa tofauti kabisa, Micho
akaondoka.
Alikuwa analipwa mshahara mzuri na Yussuf
Manji wakati huo akiwa mfadhili wa klabu kabla hajawa Mwenyekiti. Alipewa gari,
aina ya Rav4, nyumba na aliwezeshwa kwa kila alichotaka, ikiwemo kambi za nje
ya nchi, yeye mwenyewe kusafiri kwenda kuona mechi za wapinzani wake.
Naweza kusema hakuna kocha aliyewahi
kufanya katika mazingira mazuri zaidi kwa kiwango cha huduma za klabu hiyo kama
Micho.
Lakini akaamua kuaga na kuondoka. Nini
kilimkera Micho? Rahisi tu, Yanga
wajuaji sana na hawana subira. Mambo haya mawili, kama Yanga hawatabidilika,
hakuna kocha mtaalamu anayeweza kuishi nao.
Rejea mechi iliyopita ya Ligi Kuu kati ya
Yanga na Ruvu Shooting, ndani ya dakika 10 timu hiyo ya Jangwani ilikuwa
imekwishafungwa mabao 2-0 na baada ya bao la pili, makocha wa jukwaani wakaanza
kumpigia kelele kocha Ernie Brandts, wakimtaka afanye mabadiliko.
Toa Oscar, toa Oscar. Kisa tu mipira
iliyowapa mabao Ruvu ilitoka upande wa kushoto, basi kwa uelewa wao, wakajua
tatizo la timu liko kwa beki wa kushoto Oscar Joshua.
Lakini tatizo la msingi la Yanga lilikuwa
katika kiungo mkabaji siku hiyo, ambako alianzishwa Nurdin Bakari, aliyekuwa
anarejea uwanjani baada ya muda mrefu wa kuwa nje kwa sababu ya majeruhi, hivyo
kitalaamu alikuwa anakosa kitu kinaitwa uimara wa kucheza mechi.
Zile kelele zilitaka kumshinikiza kocha
Brandts kufanya mabadiliko mapema, alimuinua Juma Seif ‘Kijiko’ apashe, lakini
bahati nzuri Nurdin akarekebisha makosa yake na timu ikaimarika na kufanikiwa
kusawazisha mabao.
Timu zilikwenda kupumzika zikiwa
zimefungana mabao 2-2 na mwisho wa mchezo Yanga ikashinda 3-2.
Naweza kusema siku hiyo Brandts aliionja
joto ya jiwe kidogo ya mashabiki wa Yanga na hii sasa itamfanya hata katika
utendaji wake awafikirie mashabiki hao, hivyo kukosa uhuru kidogo.
Tunarudi kule kule, aliyosema Timbe kwamba
kufanya kazi Yanga ni ngumu mno, kwa sababu ya uelewa mdogo wa mashabiki na
viongozi wake.
Timbe aliwazungumzia viongozi wa Yanga
aliofanya nao kazi, ambao si hawa. Alifanya kazi chini ya Mwenyekiti, Wakili
Lloyd Nchunga na sasa Brandts anafanya kazi chini ya Mwenyekiti ‘Alhaj
Mtarajiwa’ Yussuf Manji.
Mimi naamini ukocha ni mgumu sana haswa kwa
huku kwetu Afrika, hususan nchi yetu hii Tanzania, ambayo wachezaji wake wengi
hawana malengo na uelewa wao ni tatizo zaidi.
Hao makocha wa Ulaya wenyewe, pamoja na
kufanya kazi na wachezaji waelewa, bado ukiwaomba maoni yao kuhusu kazi yao,
watakuambia ni ngumu.
Kinachonikera zaidi kwa sisi Watanzania ni
ujuaji wetu. Tunajua sana. Mkute Mtanzania baa anavyomkosoa Jose Mourinho, Alex
Ferguson, Arsene Wenger au Brendan Rodgers, utachoka. Yaani sisi tunajua sana
na ninadhani Mwalimu Nyerere aliona mbali sana hata akahakikisha baadhi ya vitu
hatuvipati mapema, maana ingekuwa hatari zaidi.
Nataka niwaambie kitu kimoja wana Yanga,
najua fikra zao ni kushindana na Azam na Simba, lakini hilo silo jukumu
walilompa Brandts. Wamempa Mholanzi huyo jukumu la kuwatengenezea timu bora na
ya ushindani hadi kufika mwaka 2014 iwe tayari kwa mashindano ya Afrika.
Hata yeye Brandts anajua ana wajibu wa
kuiongoza vema timu katika Ligi Kuu, lakini yeye ana hesabu na mipango yake
ambayo mashabiki hawaijui. Kwa sababu hiyo, mashabiki na viongozi wa Yanga
waache kuingia kichwani mwa kocha.
Yanga walitafuta kocha na wakajiridhisha
kwamba Brandts ndiye anayewafaa baada ya kupitia wasifu wa makocha kadhaa, sasa
haiwezekani baada ya mechi tatu waanze kumuingilia katika kazi yake.
Ona sasa, walitaka Joshua atolewe na
hakutoka na timu ikashinda, tena akicheza dakika zote 90. Yanga wasimfikishe mahala Brandts naye
akaamini kufanya kazi Yanga ni vigumu. Alamsiki.