KAMATI ya Sheria, Maadili na Hadhi
za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), itakutana tena kujadili
hatua za kuichukulia klabu ya Yanga kwa kukaidi agizo la kuilipa Simba SC fedha
alizochukua mchezaji wao, Mbuyu Twite dola za Kimarekani 32,000.
Na Mahmoud Zubeiry |
Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj
Ismail Aden Rage alipanda ndege hadi Kigali, Rwanda na kumsainisha fomu za
mkataba wa usajili beki wa APR wakati huo, Mbuyu Twite sambamba na kumpa fedha
taslimu dola za Kimarekani 30,000.
Kimsingi Mbuyu Twite alikubali
kujiunga na Simba, lakini wakati Rage anamalizana na beki huyo mwenye asili ya
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), tayari kiongozi wa Yanga, Abdallah
Ahmed Bin Kleb alikuwa Kigali kwa lengo la kumsajili pia beki huyo.
Rage alipomalizana na Twite, akapiga
naye picha na kurejea Dar es Salaam kuzionyesha akiamini mchezaji atakuja
baadaye. Kumbe, nyuma yake Bin Kleb akaenda kumbadili mawazo Twite na kusaini
pia Yanga, aliyojiunga nayo.
Kwa kuwa Simba waliondoka Rwanda
bila kukamilisha taratibu za usajili, kama kuzungumza na klabu yake, Yanga huko
nyuma wakakamilisha taratibu zote. Na kumbe yule mchezaji alikuwa anacheza kwa
mkopo APR kutoka FC Lupopo ya DRC, Yanga ikaenda kumnunua kwa klabu yake
halisi.
Twite akakabidhi fedha alizopewa na
Rage kwa viongozi wa Lupopo wazirudishe Simba. Awali, Simba walizikataa fedha
hizo, kwa sababu bado walikuwa wana nia na mchezaji, hivyo bado walikuwa kwenye
mapambano ya kumuwania.
Hata hivyo, baadaye
walipojiridhisha hawawezi kumpata tena, wakaamua kuachana naye na kutaka
warudishiwe fedha zao tu. Hii ilikuja baada ya Kamati ya Sheria na Maadili
kumuidhinisha mchezaji huyo Yanga, Septemba 10, mwaka huu lakini ikaamuru fedha
alizochukua Simba zirudishwe ndani ya siku 21, ambazo ziliisha Oktoba 3, mwaka
huu.
Lakini hadi leo, Yanga imeshindwa
kuonyesha ushirikiano kwa kulipa fedha hizo na kwa sababu hiyo, Mwenyekiti wa
Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za Wachezaji ya Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), Wakili Alex Mgongolwa amesema kwamba Kamati yake itakutana tena hivi
karibuni, kujadili hatua za kuichukulia klabu ya Yanga kwa kukaidi agizo la
kuilipa Simba SC fedha alizochukua mchezaji wao, Mbuyu Twite dola za Kimarekani
32,000.
Mgongolwa alisema kwamba tayari
amekwishamuagiza Katibu wa TFF, Angetile Osiah aitishe kikao cha Kamati hiyo,
kujadili zaidi sakata hilo.
“Tutakutana kujadili na kuamua
hatua za kuchukua, unajua maamuzi ya awali ya Kamati, yalikuwa Yanga walipe
hizo fedha hadi kufika Oktoba 3, lakini kwa kuwa wameshindwa kufanya hivyo,
inabidi Kamati ikutane tena kujadili hatua za kuchukua.
Ndiyo maana hata wale waliotaka
Yanga wakatwe fedha hizo katika mapato yao ya milangoni, ilishindikana kwa kuwa
hayo hayakuwa maamuzi ya Kamati yetu,”alisema Mgongolwa. Kamati hiyo ambayo
itakutana tena inaundwa na Mgongolwa, Hussein Mwamba, Imani Madega, Rage, Lloyd
Nchunga na Omari Gumbo.
Hakika kitu wanachokifanya Yanga
sasa si uungwana katika suala hili la Twite. Tayari Yanga walikwishaiumiza
Simba kwa kuingilia usajili wa beki huyo- pekee hiyo ilitosha, lakini bado
wanataka kuwaumiza zaidi wenzao kwa kukwepa kulipa fedha hizo. Huu si uungwana.
Kwa upande wao, Yanga kama klabu
kubwa yenye viongozi wenye heshima kubwa, wanapaswa kutambua wanajishushia
heshima yao na heshima ya klabu yao pia kwa hili wanalolifanya.
Lakini pia, hii inaweza kuiweka
pabaya klabu, iwapo Kamati ya Mgongolwa itaamua kuchukua hatua kali. Kitendo
cha kupuuza maagizo halali ya Kamati hiyo, tena bila maelezo yoyote ni kosa kwa
mujibu wa sheria na kwa hatua yoyote watakayochukuliwa Yanga hawataonewa.
Lakini kwa nini ifikie huko? Hii
ndiyo Yanga ambayo inakabiliwa na madai mengine, yaliyofikishwa hadi Shirikisho
la Soka la Kimataifa (FIFA) yanayohusu dhuluma za malipo ya waajiri wake,
wakiwemo makocha na wachezaji.
Nadhani Yanga hawajui moto
wanaouchezea una makali kiasi gani hadi uwachome.
Kocha wao wa zamani, Kostadin
Bozidar Papic amefungua mashitaka FIFA, dhidi ya klabu hiyo, akidai malimbikizo
yake ya mishahara, dola za Kimarekani 12,300, zaidi ya Sh. Milioni 15 za
Tanzania.
Na Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), kupitia kwa Katibu wake, Angetile Osiah Malabeja limekwishawaonya Yanga
juu ya hili, baada ya kupokea barua kutoka Kitengo cha Sheria cha FIFA,
kikiwataka kuitaarifu Yanga kuhusu mashtaka yaliyowasilishwa na kocha wao huyo
zamani.
Angetile alisema katika malalamiko
yake, Papic anadai kuwa hajalipwa malimbikizo ya mshahara wake yanayofikia
kiasi cha dola 12,300 za Kimarekani na alikuwa akiwasiliana na maofisa na
viongozi waYanga, lakini hakupata ushirikiano na hivyo kuamua kwenda FIFA.
Angetile alisema TFF ilifanya
juhudi za kuwasiliana na Yanga kuhusu malalamiko hayo ili kujaribu kumzuia
kocha huyo asishtaki FIFA, lakini juhudi hizo hazikuzaa matunda.
“Na kama chombo kinachosimamia
uendeshaji wa soka nchini, TFF imesikitishwa na habari hizo na inaiomba klabu
ya Yanga kufanya kila jitihada kuhakikisha kuwa inawasilisha taarifa zote
muhimu na nyaraka zinazohusiana na stahiki za kocha huyo ili kama
ilishamalizana naye, sifa ya klabu ya Yanga isafishwe,”alisema Angetile.
Alisema tayari wamekwishaiandikia
barua Yanga kuitaka itekeleze utashi huo mapema iwezekanavyo.
“Tukio hilo, si tu linachafua sifa
ya klabu ya Yanga, bali soka ya Tanzania kwa ujumla kutokana na ukweli kwamba
ikishadhihirika kuwa kuna tatizo la malipo ya makocha nchini, ni dhahiri kuwa
itakuwa ni vigumu kwa klabu zetu na hata timu za taifa kupata makocha wazuri
kutoka nje kwa kuwa watakuwa wamejengeka hofu ya kufanya kazi nchini,”alisema.
Hili ni tukio la pili kwa Yanga
baada ya mchezaji wake mwingine, John Njoroge kuishtaki klabu hiyo FIFA na kushinda
kesi yake iliyoamuliwa mwezi Januari na Kitengo cha Usuluhishi wa Migogoro cha
FIFA.
Alisema ushindi wa Njoroge
unamaanisha kuwa iwapo Yanga itashindwa kutekeleza kumlipa mchezaji huyo kasi
cha Sh milioni 17, inaweza kujikuta katika adhabu ambayo itailazimisha TFF
kuishusha daraja; kuinyang’anya pointi kwa kiwango kitakachotajwa na FIFA;
kuipiga faini au adhabu zote kwenda kwa pamoja.
Sasa madai haya ya Papic, Njoroge
na ikumbukwe pia wapo makocha na wachezaji wengine hawakuondoka vizuri Yanga- hii
ni sifa mbaya kwa klabu hiyo, ambayo viongozi wa sasa wanapaswa
kuibadilisha.
Leo Simba wakiamua kuandika kitu
kama taarifa tu kwa FIFA juu ya kile walichofanyiwa na Yanga katika suala zima
la Twite- itaiweka katika wakati mgumu sana klabu hiyo. Sasa, FIFA ikirejea
kwenye rekodi zake ikakuta mafaili ya Papic na Njoroge, unaweza kuona ni hatari
ipi inawakabili Yanga.
Yanga ni klabu ya kiungwana, hiyo
ndio asili yake. Ni klabu yenye historia kubwa katika nchi hii. Ina heshima
kubwa, tena sana. ipo haja kubwa sana ya kuyalinda yote, kwa kujiepusha na
fedheha zenye kuepukika kama hizi za kudhulumu dhulumu. Haipendezi.