Na Prince Akbar
WADHAMINI wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara, kampuni ya Vodacom
Tanzania, wameikubalia klabu ya Yanga kutotumia jezi zenye nembo nyekundu na
kuipa nembo tatu ichague mojawapo, ambazo hazina rangi nyekundu.
Nembo hizo ni njano na nyeusi, kijani na nyeusi na nyeupe na
nyeusi, ambazo Yanga itatakiwa kuchagua mojawapo kutumia katika Ligi Kuu.
Yanga walikuwa wana mgomo wa kutumia nyembo nyekundu, ambayo
ndio nembo kuu ya kampuni hiyo kwa sasa na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), Leodegar Chillah Tenga akasema wanawaachia Vodacom watumie busara
kumalizana na klabu ya Yanga, juu ya mgogoro wao kuhusu nembo ya ligi hiyo.
Tenga alisema kwamba kwa kuwa msimu uliopita Vodacom
walimalizana na Yanga bila kulishirikisha shirikisho lake, na mwaka huu
wanawaachia pia.
“Kitendo kilichofanywa na Vodacom mwaka jana, kumalizana na
Yanga bila kutushirikisha kuhusu utata wa nembo, sisi tulijua kitaleta matatizo
baadaye, na kweli sasa yametokea, na ndiyo maana unaweza kuona, sekretarieti
yetu inalipeleka taratibu hili suala,”alisema Tenga.
Tenga alisema Vodacom ingewaacha TFF msimu uliopita
wakaihukumu Yanga kwa mujibu wa kanuni, hata msimu huu ingekuwa rahisi kwao
kuingilia, lakini kwa kuwa msimu uliopita waliingilia na wakaibadilishia klabu
hiyo nembo, basi na msimu huu pia wanawaachia wamalizane wenyewe.
Hatua hiyo ya Vodacom kuibadilishia Yanga nembo ya jezi,
inakuja siku mbili baada ya Wazee wa klabu hiyo, kutoa tamko la kusema wapo
tayari klabu hiyo ishushwe daraja kwa mujibu wa kanuni, lakini si kuvaa nembo
nyekundu.