Mwalusako akizungumza na Waandishi wa Habari Jangwani leo |
Na Mahmoud Zubeiry
KATIBU wa Yanga, Lawrence Mwalusako amesema kwamba timu yao
ilifungwa kimchezo na labda kwa mbinu nyingine kwenye mechi ya jana dhidi ya
Kagera Sugar, lakini si kwa sababu ya malazi mabaya wala lishe mbovu.
Mwalusako aliyezungumza na Waandishi wa Habari ‘hivi punde’
makao makuu ya klabu hiyo, makutano ya mitaa ya Twiga na Jangwani, alikuwa
anakanusha habari zilizoandikwa na gazeti moja leo, kwamba wachezaji wake walilala
wawili wawili kitanda kimoja mjini Bukoba.
“Hizi habari si kweli, wachezaji wetu walilala vizuri tu, tunasikitishwa
na habari za kizushi kama hizi, tunapenda kukanusha kwa nguvu zote,”alisema.
Mwalusako alisema kufungwa kwao Kagera kumetokana na matokeo
ya kawaida ya mchezo na sasa kuelekea mechi ya Alhamisi dhidi ya Toto African
mjini Mwanza wataongeza nguvu.
“Kuna viongozi wataenda Mwanza kuongeza nguvu, ili kuhakikisha
tunashinda mechi hiyo, wanakwenda kwa ajili ya kuwahamasisha wachezaji,”alisema
Mwalusako.
Bao pekee la
Themi Felix katika dakika ya 67, jana liliwapa Kagera Sugar ushindi wa 1-0
dhidi ya Yanga SC, kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba katika mchezo wa Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara.
Felix
aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Mnigeria, Enyinna Darlington kwa
kumtungua bao hilo, kipa Mghana wa Yanga, Yaw Berko, ameendeleza rekodi yake
kuvifunga vigogo, Simba na Yanga katika Uwanja huo.
Hiyo inakuwa
mechi ya pili Yanga kufungwa ndani ya mechi sita walizocheza hadi sasa na mbili
wametoka sare- maana yake inabaki na pointi zake nane na kuzidi kujipunguzia
matumaini ya ubingwa msimu huu, ikiwa sasa inazidiwa pointi nane na vinara wa
ligi hiyo Simba SC.
Aidha, hii
ni mechi ya pili Yanga inacheza chini ya kocha wake mpya, Mholanzi Ernie
Blandts aliyerithi mikoba ya Mbelgiji, Tom Saintfiet na katika mechi hizo mbili
ameambulia pointi moja kutokana na sare dhidi ya Simba Jumatano.
Kwa ujumla
Yanga haijashinda hata mechi moja ya ugenini kati ya tatu ilizocheza hadi sasa,
ilitoka 0-0 na Prisons, ikafungwa 3-0 na Mtibwa na jana imechapwa 1-0 na Kagera
Sugar, wakati Alhamisi itacheza na Toto African mjini Mwanza.
Katika mechi
hiyo ya jana, Yanga ilipata pigo dakika ya 23 baada ya mshambuliaji wake mahiri
na tegemeo, Said Bahanuzi ‘Spider Man’ kuchanika nyama za paja dakika ya 23,
baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea
na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete.
Tangu
ajiunge na Yanga akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, leo Bahanuzi amecheza mechi
ya 13 kwa dakika hizo 23 na ameifungia timu hiyo jumla ya mabao 12, matatu kati
ya hayo kwa penalti.
Mchezaji wa yanga Oscar Joshua akiwa ndani ya chumba chake.
Wachezaji wa timu ya Yanga, Omega Seme kulia na Frank Domayo kushoto wakiwa wamejipumzisha ndani ya vyumba vyao. Je, huu ni mzungu wa nne?
Mchezaji wa yanga Oscar Joshua akiwa ndani ya chumba chake.
Wachezaji wa timu ya Yanga, Omega Seme kulia na Frank Domayo kushoto wakiwa wamejipumzisha ndani ya vyumba vyao. Je, huu ni mzungu wa nne?