Yanga SC |
Na Mahmoud Zubeiry
KIKOSI cha Yanga
kilichoingia kambini jana katika hoteli ya Uppland, Changanyikeni, Dar es
Salaam kinaendelea vizuri na maandalizi ya mchezo wake ujao wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Ruvu Shooting Jumamosi wiki hii kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam.
Pamoja na kuweka kambi Changanyikeni, lakini Yanga inafanya
mazoezi kwenye Uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
Beki Kevin Yondan aliyeumizwa na kiungo wa Simba, Haruna
Moshi ‘Boban’ katika mechi baina ya wapinzani hao wa jadi, Oktoba 3, mwaka huu,
anaendelea vizuri na mazoezi mepesi sawa na mshambuliaji Said Bahanuzi
aliyekuwa anasumbuliwa na maumivu ya nyama za paja.
Bahanuzi
‘Spider Man’ alichanika nyama za paja la mguu wa kulia katika mechi ya Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba
Jumatatu wiki iliyopita.
Bahanuzi
aliumia dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar
na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete
katika mechi ambayo Yanga ililala 1-0, beo pekee la Themi Felix.
Bahanuzi
ndiye tegemeo la mabao la Yanga kwa sasa, kwani tangu ajiunge na timu hiyo
akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, ameifungia mabao 12 katika mechi 13, ikiwemo
ile dhidi ya Kagera aliyocheza kwa dakika 23 kabla ya kuumia na kutoka.
Yanga kwa
sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 11,
baada ya kucheza saba, kushinda tatu, sare mbili na kufungwa mbili.
Simba
iliyocheza mechi saba pia, inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 17, ikifuatiwa
na Azam FC yenye pointi 16, iliyocheza mechi sita.