Yanga SC |
Na Prince Akbar
LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo,
kwa mabingwa wa kihistoria wa ligi hiyo, Yanga SC kumenyana na Ruvu Shooting ya
Pwani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.15 jioni.
Awali mechi hiyo ilikuwa ichezwe kwenye Uwanja wa Chamazi,
lakini kufuatia ombi la Ruvu ihamishiwe Uwanja wa Taifa, Kamati ya Ligi ya TFF,
imekubali kwa sababu pia leo hakuna mechi nyingine Uwanja wa Taifa.
Katika mechi hiyo, itakayochezeshwa na refa Amon Paul kutoka
Mara ni viingilio vitakuwa Sh. 5,000 viti vya kijani na bluu, Sh. 8,000 viti
vya rangi ya chungwa, Sh. 15,000 VIP B na C na sh. 20,000 kwa VIP A.
Katika mchezo wa leo, Yanga itawakosa nyota wake beki Kevin Yondan na mshambuliaji
Said Bahanuzi kwa sababu bado hawajawa fiti.
Wawili hao
ambao ni majeruhi, wapo kwenye programu ya mazoezi mepesi na hadi jana hakuna
mmoja kati yao aliyekuwa tayari kuanza programu kamili ya mazoezi ya kocha
Mholanzi, Ernie Brandts.
Maana yake,
Mbuyu Twite ataendelea kucheza pamoja na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika beki
ya kati, wakati Jerry Tegete ataendelea kucheza na Didier Kavumbangu katika
safu ya ushambuliaji.
‘Dogo’ Simon
Msuva amemaliza adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa Oktoba 3, mwaka huu katika
mechi dhidi ya Simba na Hamisi Kiiza amerejea kutoka Uganda,
alipokwenda kuichezea timu yake ya taifa, The Cranes katika mchezo wa marudiano
wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika mwakani
nchini Afrika Kusini.
Uganda ilitolewa na Zambia kwa mikwaju ya penalti baada ya
sare ya jumla ya 1-1, Zambia wakianza kushinda nyumbani 1-0 na Uganda
wakashinda kwao 1-0 pia mwishoni mwa wiki, hivyo mchezo kuhamia kwenye mikwaju
ya penalti, ambako timu ya Kiiza ilitolewa.
Yanga iliyoweka kambi katika hoteli ya Uplands, Changanyikeni,
Dar es Salaam, imekuwa ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa shule ya sekondari ya
Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
Beki Kevin Yondan aliumizwa na kiungo wa Simba, Haruna Moshi
‘Boban’ katika mechi baina ya wapinzani hao wa jadi, Oktoba 3, mwaka huu, wakati
Bahanuzi ‘Spider Man’ alichanika
nyama za paja la mguu wa kulia katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba Oktoba 8, mwaka huu.
Bahanuzi
aliumia dakika ya 23, baada ya kugongana na beki Benjamin Effe wa Kagera Sugar
na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake ikichukuliwa na Jerry Tegete
katika mechi ambayo Yanga ililala 1-0, beo pekee la Themi Felix.
Bahanuzi
ndiye tegemeo la mabao la Yanga kwa sasa, kwani tangu ajiunge na timu hiyo akitokea
Mtibwa Sugar msimu huu, ameifungia mabao 12 katika mechi 13, ikiwemo ile dhidi
ya Kagera aliyocheza kwa dakika 23 kabla ya kuumia na kutoka.
Yanga kwa
sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi Kuu kwa pointi zake 11,
baada ya kucheza saba, kushinda tatu, sare mbili na kufungwa mbili.
Simba
iliyocheza mechi nane, inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 18, ikifuatiwa na
Azam FC yenye pointi 17, iliyocheza mechi saba.
Ruvu
Shooting inayofundishwa na Nahodha wa zamani wa Yanga, Charles Boniface Mkwasa
imekuwa ikizitoa jasho timu kongwe, Simba na Yanga inapokutana nazo katika
miaka ya karibuni.
Mechi nyingine za leo, Coastal Union itakuwa mwenyeji wa
Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga, ambayo itachezeshwa na refa
Israel Nkongo atakayesaidiwa na Hamis Chang’walu na Omari Kambangwa, wote
kutoka Dar es Salaam.
Ligi hiyo itaendelea tena Jumapili kwa mechi tatu, JKT Ruvu
itaonyeshana kazi na JKT Oljoro kwenye Uwanja wa Chamazi, Mgambo Shooting
itaikaribisha Simba kwenye Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga wakati Tanzania
Prisons na Toto Africans zitapimana ubavu kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya
Sokoine jijini Mbeya.