Msuva kushoto na Domayo kulia, wakimpongeza Kavumbangu kufunga bao la pili |
Na Mahmoud Zubeiry
YANGA SC imeendeleza wimbi la ushindi katika Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara baada ya jioni ya leo kuichapa Mgambo JKT ya Handeni,
Tanga mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Ushindi huo, unaifanya Yanga sasa iwe na pointi sawa na
mabingwa watetezi, Simba SC waliotoa sare ya 1-1 na Polisi mjini Morogoro leo,
ingawa inazidiwa bao moja tu katika wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Hadi mapumziko, Yanga walikuwa mbele kwa mabao 2-0,
yaliyotiwa kimiani na beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na mshambuliaji Didier
Kavumbangu.
Cannavaro alifunga kwa kichwa akiunganisha krosi ya Oscar
Joshua dakika ya pili kutoka wingi ya kulia, wakati Kavumbangu alimalizia pasi
ya Hamisi Kiiza dakika ya 39.
Pamoja na kutoka uwanjani wamelowa kipindi cha kwanza, lakini
Mgambo JKT walicheza soka ya kuvutia na mara mbili walikaribia kufunga kupitia
kwa Juma Mwinyimvua.
Yanga walicheza vema dakika 45 za kipindi cha kwanza, tofauti
sana na mechi za awali ambazo wamekuwa ‘wakichezewa’ sana na wapinzani.
Ilishuhudiwa katika kipindi hicho, Yanga wakimiliki zaidi
mpira na kupeana pasi za uhakika, ingawa mashambulizi yao mengi walipitisha
pembeni, hasa upande wa kulia.
Hamisi Kiiza, Msuva na Kavumbangu walicheza kwa uelewano
mkubwa pale mbele na kulitia misukosuko haswa lango la Mgambo.
Kipindi cha pili, Yanga walirudi na moto wao tena na
kuendelea kuwachachafya Mgambo.
Hata hivyo, iliwachukua Yanga dakika 34 kupata bao la tatu,
mfungaji akiwa ni Jerry Tegete aliyeingia dakika ya 68 kuchukua nafasi ya
Kavumbangu.
Tegete alifunga bao hilo akiunganisha krosi maridadi ya beki
wa kushoto, Oscar Joshua.
Pamoja na kufungwa, Mgambo waliendelea kusukuma mashambulizi
langoni mwa Yanga, ingawa leo mabeki wa timu hiyo, inayofundishwa na Mholanzi,
Ernie Brandts walicheza kwa uelewano mkubwa na kudhibiti hatari zote langoni
mwao.
Mgambo inayofundishwa na Mohamed Kampira, ilipata pigo dakika
ya 85, baada ya beki wake wa kulia, Salum Mlima kutolewa kwa kadi nyekundu ya
moja kwa moja kwa kumchezea rafu mbaya Mbuyu Twite.
Baada ya mchezo huo, Brandts alisema dakika 10 za mwanzo timu
yake ilikuwa inashindwa kumalizia vizuri mashambulizi yake, lakini baadaye
ikatulia na hatimaye kupata ushindi huo, ambao ameufurahia kwani unamuweka
katika nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Kwa upande wake, Kampira wa Mgambo alisema kufungwa ni sehemu
ya mchezo, akawasifu Yanga kwa kutumia nafasi walizopata, huku akijutia nafasi
walizopoteza wachezaji wake leo.
Kikosi cha Yanga leo kilikuwa; Ally Mustafa ‘Barthez’,
Nsajigwa Shadrack/Kevin Yondan dk 46, Oscar Joshua, Mbuyu Twite, Nadir Haroub
‘Cannavaro’, Athumani Iddi ‘Chuji’, Simon Msuva, Frank Domayo/Nurdin Bakari dk
76, Didier Kavumbangu/Jerry Tegete dk68, Hamisi Kiiza na Haruna Niyonzima.
Mgambo JKT; Godson Mmasa, Salum Mlima, Yassin Awadh, Salum
Kipanga/Godfrey Komba dk80, Bakari Mtama, Ramadhani Malima, Chande Magoja,
Mussa Ngunda, Issa Kandulu/Nassor Gumbo dk 60, Fully Maganga na Juma Mwinyimvua/Omar
Matwiko dk76.
Katika mchezo wa utangulizi, timu ya vijana chini ya umri wa
miaka 20 ya Yanga, imeifunga Mgambo JKT ya vijana pia 1-0, bao hilo pekee la
Clever Charles dakika ya 65.
Katika mechi nyingine, Simba ilitoka sare ya 1-1 Polisi
kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, wenyeji wakitangulia kupata bao dakika ya
35 kupitia kwa Mokili Rambo kabla ya Amri Kiemba kusawazisha dakika ya 57.