Yanga SC |
Na Mahmoud Zubeiry
LIGI Kuu ya Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo kwa
mechi nne za raundi ya tisa huku Azam ikiusaka usukani wa ligi hiyo ikiwa
mwenyeji wa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Kipre Herman Tchetche, tegemeo la Azam |
Mechi hiyo namba 60 ambayo kama Azam itashinda itafikisha
pointi 20, hivyo kuwa kileleni mwa Ligi Kuu ya Vodacom itakayochezwa Uwanja wa
Chamazi, Dar es Salaam, viingilio vyake vitakuwa ni Sh. 3,000 kwa sh. 10,000.
Lakini macho na masikio ya wengi yatakuwa kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam ambao Yanga wataikaribisha Polisi Morogoro, wanaoshika
mkia kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Katika mechi hiyo ambayo viingilio vitakuwa Sh. 5,000, Sh.
8,000, Sh. 15,000 na Sh. 20,000, refa Alex Mahagi kutoka Mwanza ndiye
atakayepuliza filimbi kwenye mechi hiyo namba 62, akisaidiwa na Frank Komba na
Michael Mkongwa, wote kutoka Iringa wakati mwamuzi msaidizi ni Oden Mbaga
anayetambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) wa Dar es Salaam.
Katika mechi hiyo, Yanga itawakosa mabeki wake wa kati, Job
Ibrahim, Kevin Yondan na
mshambuliaji Said Bahanuzi ambao ni majeruhi.
Job, ambaye amekuwa beki wa akiba tangu mwanzoni mwa msimu,
aliumia kifundo cha mguu mazoezini mwishoni mwa wiki na juzi hakufanya mazoezi
kabisa, wakati Yondan na Bahanuzi wanaendelea na programu ya mazoezi mepesi,
chini ya kocha Mholanzi, Ernie Brandts.
Kwa sababu hiyo, Mbuyu Twite ataendelea kucheza pamoja na
Nadir Haroub ‘Cannavaro’ katika beki ya kati, wakati Jerry Tegete ataendelea
kucheza na Didier Kavumbangu katika safu ya ushambuliaji.
‘Dogo’ Simon Msuva amemaliza adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa
Oktoba 3, mwaka huu katika mechi dhidi ya Simba na ilikuwa aanze kucheza tangu
Jumamosi, ila kutokana na kiwango duni cha Hamisi Kiiza alichoonyesha kwenye
mechi na Ruvu Shooting Jumamosi, leo kinda huyo anaweza kurudishwa uwanjani.
Kiiza aliichezea Yanga kwa mara ya kwanza siku hiyo akitokea
benchi kipindi cha pili, tangu atolewe kipindi cha kwanza katika mechi dhidi ya
Simba, Oktoba 3, mwaka huu. Kiiza alikuwa
kwao, Uganda, alipokwenda kuichezea timu yake ya taifa, The Cranes
katika mchezo wa marudiano wa kuwania tiketi ya kucheza Fainali za Kombe la
Mataifa ya Afrika mwakani nchini Afrika Kusini.
Uganda ilitolewa na Zambia kwa
mikwaju ya penalti baada ya sare ya jumla ya 1-1, Zambia wakianza kushinda
nyumbani 1-0 na Uganda wakashinda kwao 1-0 pia mwishoni mwa wiki, hivyo mchezo
kuhamia kwenye mikwaju ya penalti, ambako timu ya Kiiza ilitolewa.
Yanga imeweka kambi katika hoteli
ya Uplands, Changanyikeni, Dar es Salaam huku ikiendelea kufanya mazoezi kwenye
Uwanja wa shule ya sekondari ya Loyola, Mabibo, Dar es Salaam.
Yondan aliyeumizwa na kiungo wa
Simba, Haruna Moshi ‘Boban’ katika mechi baina ya wapinzani hao wa jadi, Oktoba
3, mwaka huu, wakati Bahanuzi
‘Spider Man’ alichanika nyama za paja la mguu wa kulia katika mechi ya Ligi Kuu
ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba
Oktoba 8, mwaka huu.
Bahanuzi aliumia dakika ya 23, baada ya kugongana na beki
Benjamin Effe wa Kagera Sugar na kushindwa kuendelea na mchezo, nafasi yake
ikichukuliwa na Jerry Tegete katika mechi ambayo Yanga ililala 1-0, beo pekee
la Themi Felix.
Bahanuzi ndiye tegemeo la mabao la Yanga kwa sasa, kwani
tangu ajiunge na timu hiyo akitokea Mtibwa Sugar msimu huu, ameifungia mabao 12
katika mechi 13, ikiwemo ile dhidi ya Kagera aliyocheza kwa dakika 23 kabla ya
kuumia na kutoka.
Yanga kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi
Kuu kwa pointi zake 14, baada ya kucheza nane, kushinda nne, sare mbili na
kufungwa mbili. Simba iliyocheza mechi tisa,
inaongoza ligi hiyo kwa pointi zake 19, ikifuatiwa na Azam FC yenye pointi 17,
iliyocheza mechi saba.
Kwenye Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga, wenyeji Coastal Union
wataikaribisha African Lyon ya Dar es Salaam, wakati Mtibwa Sugar itaikaribisha
Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Manungu ulioko kwenye mashamba ya miwa Turiani
mkoani Morogoro.