Kikosi cha Yanga |
Na Prince Akbar
LIGI Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara inatarajiwa kuendelea leo kwa mchezo mmoja tu, ambao ni
kiporo cha jana, kati ya mabingwa wa kihistoria wa ligi hiyo, dhidi ya wenyeji
Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Yanga iko
Bukoba tangu Ijumaa asubuhi, lakini mechi hiyo iliahirishwa kutoka jana hadi
leo kutokana Uwanja wa Kaitaba kukabiliwa na shguhuli nyingine ya kijamii.
Yanga jana
ilifanya mazoezi yake ya mwisho kwenye Uwanja wa Kaitaba jioni na kocha
Mholanzi, Ernie Blandts amesema kikosi chake kipo tayari kwa mchezo wa leo. Kagera
ambayo inafundishwa na gwiji wa zamani wa soka Tanzania, Abdallah Kibadeni imetamba
kuifunga Yanga leo.
Hadi sasa,
mwenendo wa Yanga si mzuri katika ligi hiyo, ikiwa imecheza mechi tano,
kufungwa moja, sare mbili na kushinda mbili na inazidiwa pointi nane na
wapinzani wao wa jadi, Simba SC wanaoongoza ligi hiyo. Kwa sababu hiyo, Yanga
inahitaji lazima ushindi katika mchezo wa leo, ili kujiimarisha katika mbio za
ubingwa, ambazo wapinzani wake wakuu Simba na Azam wanaonekana kujipanga vema
tangu mwanzo.
Katika mechi
zilizochezwa jana, Simba SC ilizidi kujiimarisha kileleni kufuatia ushindi wa
mabao 4-1 ilioupata kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya JKT Oljoro
ya Arusha, ambayo ilimaliza pungufu ya wachezaji wawili baada ya kipa wake
Shaibu Issa na mshambuliaji Meshack Nyambele kutolewa kwa kadi nyekundu kipindi
cha pili.
Katika mechi
hiyo iliyochezeshwa na refa Amon Paul wa Mara, aliyesaidiwa na Anold Bugabo wa
Singida na Charles Simon wa Dodoma, hadi mapumziko Simba walikuwa tayari mbele
kwa mabao 2-1, mabao yake yote yakitiwa kimiani na kiungo Amri Ramadhan Kiemba
katika dakika za 16 na 44, wakati la Oljoro lilifungwa na Paul Nonga dakika ya
29.
Kiemba
alifunga bao la kwanza akiunganisha krosi pasi ya Christopher Edward, wakati
bao la pili lilitokana na krosi ya Nassor Masoud ‘Chollo’, yote kutokana na
mashambulizi ya upande wa kulia.
Ilikuwa
rahisi kwa Kiemba kufunga mabao yote akiwa kwenye eneo la hatari, kutokana na
mabeki wa Oljoro kumuwekea ulinzi zaidi Felix Sunzu.
Nonga naye
alifunga bao lake baada ya kupewa pasi ndefu na kumpiga chenga kipa na Nahodha
wa Simba, Juma Kaseja upande wa kulia mwa Uwanja na kuutumbukiza mpira nyavuni
kiulaini.
Bao hilo
lilitokana na beki Paul Ngalema kupokonywa mpira wakati amepanda kusaidia
mashambulizi na Oljoro wakafanya shambulizi la haraka.
Kipindi cha
pili Simba walirudi vizuri zaidi uwanjani na kuuteka zaidi mchezo- jambo ambalo
liliwafanya Oljoro wawapunguze kasi kwa kuwachezea rafu. Hilo liliwagharimu
kupoteza wachezaji wao wawili kabla ya filimbi ya mwisho na kufungwa mabao
mawili zaidi.
Dakika ya 83
Mganda Emanuel Okwi aliifungia Simba bao la tatu na katika dakika ya tatu ya
muda wa nyongeza baada ya kutimu dakika 90 za mchezo, Okwi akiwa anaelekea
kufunga tena, alikwatuliwa na kipa wa Oljoro Shaibu Issa na refa akaamuru
penalti sambamba na kumtoa nje kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja mlinda mlango
huyo.
Awali ya
hapo, Oljoro ilimpoteza mchezaji mwingine, Nyambele dakika ya 78, ambaye
alionyeshwa njano ya pili kwa rafu aliyomchezea Jonas Mkude. Nahodha Kaseja
alitaka kwenda kupiga, lakini akazuiwa na Felix Mumba Sunzu akaenda kufunga bao
la nne kwa mkwaju wa penalti.
Kwa ushindi
huo, Simba imefikisha pointi 16 baada ya kucheza mechi sita, hivyo kuendelea
kuongoza Ligi Kuu, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 13, ingawa imecheza mechi
tano.
Katika mechi
nyingine za jana, Mgambo imepata ushindi wake wa kwanza baada ya kuichapa
Polisi Morogoro 1-0, wakati Toto African imeichapa JKT Ruvu 2-1 na Prisons
imelazimishwa sare ya bila kufungana na Mtibwa Sugar.