Brandts akiwaongoza vijana wake mazoezini |
Na Mahmoud Zubeiry
UONGOZI wa Yanga umemshauri kocha Ernie Brandts kutumia
wachezaji wote badala ya kuwasahau kabisa wengine benchi, ili uweze kubaini
wachezaji ambao hawana msaada katika timu na kuweza kuwatema katika dirisha
dogo Januari, mwakani.
Katika mechi za karibuni, Yanga ikiwatumia wachezaji tofauti
wakiwemo wale ambao wamekuwa benchi kwa muda mrefu kama Nahodha Nsajigwa Shadrack,
Nurdin Bakari na Rashid Gumbo.
Yanga imeweka mtego kwa wachezaji ambao wanaridhika kupewa
mishahara bure bila kufanya kazi na Januari watatupiwa virago.
Chanzo cha habari kutoka Yanga kimesema kwamba, klabu inataka
wachezaji washindani wa namba, ili kuongeza hamasa katika timu, badala ya kuwa
na wachezaji wengi wa mazoezi tu.
Yanga wanaonekana kucharuka sasa dhidi ya wachezaji wao kwa
ujumla, kuanzia suala la nidhamu na uwajibikaji pia, baada ya kuona wanawekeza
fedha nyingi katika usajili, lakini bado timu haichezi soka ya kuvutia, jambo ambalo
wanaona linatokana na wahezaji kubweteka.
Juzi Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yanga, Abdallah
Ahmed Bin Kleb ‘aliwawakia’ wachezaji wa mbele wa timu hiyo kwa uchoyo wa pasi
na kukemea tabia inayoonekana kuanza kujitokeza, wachezaji wa timu hiyo
kutopendana.
Bin Kleb aliingia ‘kwa hasira’ chumba cha kubadilishia nguo
cha Yanga na kuanza kufoka juu ya tabia hiyo, akisema timu inatengeneza nafasi
nyingi, lakini kwa uchoyo wa baadhi ya wachezaji kutoa pasi kwa wenzao walio
kwenye nafasi nzuri zaidi, inaambulia mabao machache.
Bosi huyo alifanya hivyo baada ya mechi dhidi ya Polisi
Morogoro kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, ambayo Yanga ilishinda 3-0.
Lakini pia Bin Kleb alimuuliza kocha Mkuu, Mholanzi Ernie
Brandts kwa nini timu haichezi vizuri pamoja na kushinda. Brandts alitumia
hekima kukwepa kujibu swali mbele ya wachezaji, lakini baadaye alimvuta pembeni
Bin Kleb wakazungumza.
Tayari kuna dalili za mgawanyiko ndani ya Yanga baina ya
wachezaji na hilo lilijidhihirisha wakati Hamisi Kiiza alipofunga bao lake
lililokuwa la tatu katika ushindi wa 3-0, hakwenda kushangilia na wachezaji
wenzake, bali alimkimbilia kipa wa akiba, Mghana Yawe Berko kushangilia naye juzi.
Ingawa hajawahi kulalamika, lakini ukiifuatailia Yanga tangu
baada ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame,
Kiiza ndiye ambaye mara nyingi amekuwa hapewi pasi na wenzake anapokuwa kwenye
nafasi nzuri, ingawa yeye amekuwa anawapa tu wenzake pasi za mabao.
Pamoja na hayo, hali hiyo inaonekana kidogo kuathiri uchezaji
wa Kiiza, anayeonekana kuwa mnyonge na asiye na raha uwanjani na haikushangaza
alipotolewa nje kipindi cha kwanza kwenye mechi dhidi ya Simba, Oktoba 3, mwaka
huu.
Lakini Kiiza amekuwa akicheza kwa kiwango cha juu mno katika
timu yake ya taifa, Uganda, The Cranes pamoja na ‘kusuasua’ Yanga.
Yanga iko Arusha tangu jana na imefikia katika hoteli ya
Joshmal, huku ikifanya mazoezi kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid tayari kwa
mechi yao ya Ligi Kuu dhidi ya wenyeji JKT Oljoro kesho kwenye Uwanja huo.
Yanga inashika nafasi ya tatu katika Ligi Kuu, ikiwa na
pointi 14, baada ya kucheza mechi tisa, nyuma ya Azam FC yenye pointi 18, baada
ya kucheza mechi nane, wakati mabingwa watetezi Simba SC, wapo kileleni kwa
pointi zao 19. Simba na Azam zitacheza kesho.