Wachezaji wa Kagera wakiwasalimia wachezaji wa JKT leo Uwanja wa Kaitaba. Picha kwa hisani ya Bukoba Sports. |
Na Prince Akbar, Bukoba
WABABE wa Yanga, Kagera Sugar jioni hii wamelazimishwa sare
ya bila kufungana na JKT Ruvu ya Pwani katika mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom
Tanzania Bara, uliofanyika kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Sare hiyo imeisaidia JKT kupanda kwa nafasi moja kutoka ya 13
hadi ya 12, juu ya JKT Mgambo ya Tanga, wakati Kagera imelingana kila kitu sasa
na Yanga, pointi na wastani wa mabao, zikiwa katika nafasi ya nne na ya tano.
Sare hii, maana yake Kagera imeshindwa kuendeleza wimbi la
ushindi waliloanza nalo juzi, wakiifunga Yanga 1-0, kwa bao pekee la Themi
Felix katika dakika ya 67 kwenye Uwanja wa Kaitaba, Bukoba.
Felix aliyeingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya
Mnigeria, Enyinna Darlington kwa kumtungua bao hilo, kipa Mghana wa Yanga, Yaw
Berko, ameendeleza rekodi yake kuvifunga vigogo, Simba na Yanga katika Uwanja
huo.
Ligi hiyo, itaendelea kesho kwa mchezo mmoja, utakaopigwa
Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza baina ya wenyeji Toto African na Yanga SC.