Azam FC; Wenye ukuta tishio zaidi Ligi Kuu |
Na Mahmoud Zubeiry
WAKATI Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara ipo katika mzunguko
wake wa tisa, hadi sasa Azam FC ndio imeonyesha kuwa timu yenye ukuta mgumu
zaidi na ikiwa kesho inamenyana na Ruvu Shooting katika mfululizo wa ligi hiyo,
imefungwa mabao mawili tu katika mechi saba.
Azam ilifungwa mabao hayo katika mechi yake ya pili, dhidi ya
wenyeji Toto African kwenye Uwanja wa CCM Kirumba mjini Mwanza na tangu hapo
imecheza dakika 450 bila kuruhusu nyavu zao kutikiswa na katika mechi zote hizo
alidaka Mwadini Ally.
Kwa kawaida safu ya ulinzi ya Azam huwa haibadiliki sana na
katika mechi zote hizo ambazo hawajafungwa, Mwadini amekuwa akilindwa na Ibrahim
Shikanda kulia, kushoto Erasto Nyoni na katikati Aggrey Morris na Said Mourad,
juu yao kiungo mkabaji Ibrahim Mwaipopo.
Unasemaje kuhusu ukuta huu, upo ukuta unaostahili kuitwa jina
gumu katika Ligi Kuu hadi sasa zaidi ya huu? Hakuna hakika.
Kasi ya ufungaji wa mabao ya Azam hadi sasa ni ya wastani wa kati,
katika mechi saba walizocheza wamefunga mabao manane, bado ni wastani wa bao
moja katika kila mechi na hii ni kwa sababu mfungaji bora wa timu hiyo, John
Bocco ‘Adebayor’ bado hajafunguka.
Kwa wenye kufuatilia rekodi ya Bocco katika Ligi Kuu, amekuwa
tishio zaidi katika mzunguko wa pili, hivyo bado hatuwezi kusema chochote juu
yake hadi sasa hadi wakati utakapofika.
Timu inayoifuatia Azam kwa kuwa na ukuta mgumu ni JKT Mgambo
Shooting, ambao wamepanda Ligi Kuu msimu huu. Timu hiyo ya Muheza, katika mechi
zake nane ilizocheza hadi sasa, imeruhusu nyavu zake kutikiswa mara nne tu,
ingawa na yenyewe pia haina makali sana ya kufunga, kwani imefunga mabao sita
tu.
Ingawa haijafunga hata bao moja katika Ligi Kuu msimu huu, Polisi
ya Morogoro iliyopanda pia Ligi Kuu msimu huu, ni timu ya tatu kwa ubora wa
beki yake hadi ligi ilipofikia, hadi sasa katika mechi zake sita wamefungwa
mabao matano tu. Hii ni timu ambayo inashika mkia katika Ligi Kuu na kesho
inamenyana na Yanga.
Prisons ya Mbeya ambayo nayo imepanda Ligi Kuu msimu huu, pia
ina ukuta mgumu, kwani katika mechi zake nane ilizocheza hadi sasa, imefungwa
mabao matano tu, ingawa nayo pia haina safu tishio sana ya ufungaji, kwani
imefunga mabao matano pia.
Tazama utaona timu zote zilizopanda Ligi Kuu msimu huu zimewekeza
vizuri katika safu zake za ulinzi- Mgambo, Prisons na Moro, zote zimefungwa
mabao machache kuliko hata vigogo Simba na Yanga waliotumia mamilioni mengi
kusajili hadi mabeki wa kigeni.
Mabingwa watetezi Simba SC, wakiwa wanaongoza kwa safu kali
zaidi ya ushambuliaji, iliyovuna mabao 16 katika mechi tisa, ndiyo wanaofuatia
kwa kuwa na ukuta mgumu, wakiwa wamefungwa mabao sita tu katika mechi hizo.
Kagera Sugar ya Bukoba ndiyo inayofuatia kuwa na ukuta mgumu,
ikiwa imefungwa mabao sita pia katika mechi zake saba na yenyewe imefunga mabao
saba.
Coastal Union ya Tanga katika mechi zake nane, pia imefungwa
mabao manane, wakati yenyewe imefunga mabao 10, sawa na JKT Oljoro ambayo
katika mechi nane pia, imefunga mabao nane, ingawa yenyewe imefunga mabao saba
wakati Mtibwa Sugar katika mechi saba imefunga mabao manane na imefungwa manane
pia.
Yanga ndiyo wanafuatia sasa kwa ‘ukuta bora’, wakiwa
wamefungwa mabao 10 katika mechi nane, ingawa hawa sasa wanaonekana pia kuwa na
safu kali ya ushambuliaji, ambayo hadi sasa imefunga mabao 14.
Hiyo ni safu ya ushambuliaji ya pili kwa ukali wa mabao,
baada ya safu ya mabingwa watetezi Simba SC, iliyofunga mabao 16 hadi sasa
katika mechi tisa.
African Lyon inafuatia kuwa na safu kali ya ulinzi, katika
mechi nane ikiwa imefungwa mabao 11 na hatari zaidi ni kwamba hata safu yake ya
ushambuliaji haitishi sana, kwani imefunga mabao matano tu.
Toto African ambayo ndio pekee inajua utamu wa nyavu za Azam
hadi sasa, nayo imefungwa mabao 11 katika mechi nane, ikiwa nayo imefunga mabao
matano tu.
Timu mbili za mkoa mmoja, Pwani, Ruvu Shooting na JKT Ruvu
ndizo ambazo zinaongoza kuwa na kuta zenye nyufa nyingi, kwani hadi sasa zimeruhusu
mabao 13 kila timu.
Ruvu Shooting pamoja na kufungwa mabao 13, angalau nayo
imeonyesha uhai katika safu yake ya ushambuliaji kwa kufunga mabao 11, lakini
JKT iliyofungwa ‘dazeni’ ya mabao na nyongeza ya bao moja, yenyewe imefunga
mabao saba tu.
Katika msimamo wa Ligi Kuu, mbio za ubingwa hadi sasa bado ni
za farasi watatu tu, Simba, Yanga na Azam zinazofukuzana kileleni, wakati kule kwenye
mlango wa kutokea, Mtibwa Sugar, JKT Ruvu, African Lyon, Toto African na Polisi
Moro zimebanana kisawasawa. Yote tisa, ukuta wa Azam umetia fora hadi sasa
katika Ligi Kuu na safu ya ushambuliaji ya Simba ndiyo inayotisha zaidi.
MSIMAMO WA LIGI KUU BARA
P W D L GF GA GD Pts
Simba SC 9 5 4 0 16 6 10 19
Azam FC 7 5 2 0 8 2 7 17
Yanga SC 8 4 2 2 14 10 4 14
Coastal 8 3 3 2 10 8 2 13
JKT Oljoro 8 2 5 2 7 8 -1 11
JKT Mgambo 8 3 2 3 6 4 2 10
Prisons 8 2 4 2 5 5 0 10
Kagera Sugar 7 2 3 2 7 6 1 9
Ruvu Shooting 8 3 0 5 11 13 -2 9
Mtibwa Sugar 7 2 2 3 8 8 0 8
JKT Ruvu 8 2 2 4 7 13 -6 8
African Lyon 8 2 1 5 5 11 -6 7
Toto African 8 1 3 4 7 11 -4 6
Polisi Moro 6 0 2 4 0 5 -5 2
(P idadi ya mechi ambazo timu imecheza, W mechi ambazo
imeshinda, D sare, L kufungwa, GF mabao iliyofunga, GA mabao iliyofungwa, GD
mabao iliyonayo ukitoa mabao iliyofungwa, -maana yake imefungwa zaidi ya ilivyofunga
na Pts ni idadi ya pointi)