Manchester City ilipata pigo baada ya mchezaji wake, David Silva kuumia dakika ya 10 na kutolewa nje akiichezea Hispania dhidi ya Ufaransa
UJERUMANI ilishikwa kutoka kuongoza 4-0 hadi kupata sare ya 4-4 na Sweden, wakati mabingwa wa dunia, Hispania walipigwa bao dakika ya mwisho na kulazimishwa sare ya 1-1 na Ufaransa, huku timu zikipoteza rekodi ya asilimia 100 katika mechi za kufuzu kwenye fainali za Kombe la Dunia jana.
Baada ya kuongoza 4-0 kutokana na mabao mawili ya Miroslav Klose na mengine ya Per Mertesacker na Mesut Ozil, Ujerumani ilitepeta na kurudishiwa mabao yote.
Sweden ilipata mabao yake kipindi cha pili kupitia kwa Zlatan Ibrahimovic na Mikael Lustig kabla ya Johan Elmander kuwaweka nyuma 4-3 dakika ya 76.
Wasweden walisawazisha dakika nne kabla ya filimbi ya mwisho kwa bao la Rasmus Elm.
Sergio Ramos aliifungia Hispania bao la kuongoza dakika ya 25 na wangeweza kupata la pili kama mkwaju wa penalti wa Cesc Fabregas usingeokolewa na Hugo Lloris na Olivier Giroud, ambaye aliingia dakika sita za mwisho, akaisawazishia Ufaransa dakika ya mwisho.
Ireland Kaskazini iliibuka ndani ya dakika 11 kumtibulia Cristiano Ronaldo katika mechi yake ya 100 akiichezea Ureno baada ya bao la kichwa la Helder Postiga kuwapa sare ya 1-1 mjini Porto.
Urusi ilifunga Azerbaijan 1-0 mjini Moscow na kuendeleza rekodi yao nzuri chini ya kocha Mtaliano Fabio Capello.
Uholanzi pia imeshinda mechi ya nne mfululizo, baada ya kuifunga Romania mabao 4-1 mjini Bucharest.
Tofauti na Hispania, Uholanzi imeendeleza wimbi la ushindi baada ya kuzima rekodi ya Romania kutofungwa kwa kuichapa 4-1 na kukamata usukani wa Kundi D.
Jeremain Lens aliwafungia Waholanzi bao la kuongoza dakika ya nane, kabla ya Bruno Martens kufunga dakika ya 28 na Rafael van der Vaart kufunga kwa penalti kabla ya mapumziko na kufanya 3-1.
Ciprian Marica aliifungia Romania dakika ya 39 lakini Robin van Persie akaongeza la nne dakika tano kabla ya filimbi ya mwisho.
Mchezo kati ya Poland na England mjini Warsaw umeahirishwa kutokana na hali ya hewa, mvua kali iliyosababisha maji kujaa uwanjani na sasa utachezwa leo.
Bosnia iliifunga Lithuania 3-0 nyumbani na kubaki kileleni mwa Kundi G pamoja na Ugiriki ambayo imeifunga Slovakia 1-0 mjini Bratislava. .
Ubelgiji imeifunga Scotland 2-0 mjini Brussels na Croatia imeifunga 2-0 Wales mjini Osijek.