Rais wa TFF, Tenga |
Na Prince Akbar
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) na Shirikisho la Soka Kenya
(FKF) wamefikia makubaliano ya kushirikiana katika maeneo mbalimbali kwa lengo
la kuinua kiwango cha mpira wa miguu katika nchi hizo.
Akizungumza baada ya mkutano uliowakutanisha vinara wa
mashirikisho hayo Dar es Salaam jana, Rais wa TFF, Leodegar Tenga amesema
wameamua kurejesha uhusiano huo uliokuwepo zamani baada ya kuwepo utulivu
katika uendeshaji mpira wa miguu nchini Kenya.
Amesema maeneo ya ushirikiano ambayo wameagiza yafanyiwe kazi
na sekretarieti za pande zote (TFF na KFF) ili baadaye yaingizwe katika Hati ya
Makubaliano (MoU) ni mafunzo, waamuzi, mechi za timu za Taifa za wakubwa,
vijana na wanawake, na Ligi Kuu.
Rais Tenga pia amesema wameamua kuwepo ziara za mafunzo
(study tours) katika maeneo mbalimbali ambapo kwa Kenya wao Ligi Kuu yao
iliingia katika mfumo wa kampuni mapema, hivyo itakuwa fursa nzuri kwa Bodi ya
Ligi Kuu ambayo iko kwenye mchakato wa kuanzishwa kupata uzoefu kwa wenzao wa
Kenya.
Naye Rais wa FKF, Sam Nyamweya aliyefuatana na Makamu wake wa
Rais, Robert Asembo amesema ushirikiano kati ya Tanzania na Kenya ni wa
kihistoria, hivyo wameamua kuuanzisha upya kwa faida ya nchi hizo.
Amesema hivi karibuni FKF ilichukua waamuzi kutoka Tanzania waliochezesha
mechi ya kirafiki kati ya Kenya (Harambee Stars) na Afrika Kusini (Bafana
Bafana), hivyo wameamua kubadilishana waamuzi kwa lengo la kuwaongezea uzoefu.
“Waamuzi wa Tanzania walichezesha vizuri mechi ile. Unajua
kwetu kuna upinzani mkubwa katika klabu kama AFC Leopards na Gor Mahia,
ukipanga refa utasikia wengine wanalalamika, mara huyo ni Mjaluo. Hata
akichezesha vizuri bado watalalamika tu kutokana na upinzani uliopo katika
klabu hizo,” amesema.
Rais Nyamweya ameongeza kuwa ili kuondoa malalamiko katika
mechi za aina hiyo wanaweza kuchukua waamuzi kutoka Tanzania, na vilevile
waamuzi kutoka Kenya wakachezesha mechi za aina hiyo nchini Tanzania.
Amesema vilevile wamepanga kuangalia uwezekano wa kuwa na
mechi za kuandaa timu kabla ya kuanza Ligi Kuu za nchi hizo ambapo washindi
watatu au wanne wa kwanza katika ligi hizo kushindana.
Kwa upande wa mafunzo, wamekubaliana kuwa kwa vile kila nchi
ina wakufunzi wanaotambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu
(FIFA) na la Afrika (CAF) watawatumia kuandaa mafunzo ya mara kwa mara kwa
waamuzi, makocha, madaktari wa tiba ya michezo na viongozi badala ya kusubiri
mafunzo ya aina hiyo kutoka kwa mashirikisho hayo ya kimataifa.