MZUNGUKO wa kwanza wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
unaelekea ukingoni na hadi leo hakuna chochote kilichosemwa na viongozi wa
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhusu michuano ya Kombe la FA.
Na Mahmoud Zubeiry |
Katika kalenda ya mwaka huu ya matukio ya TFF, michuano ya FA
iliorodheshwa, lakini wasiwasi unaanza kuja kwa sababu hata Kombe la Taifa
liliorodheshwa nalo halikufanyika pia na hadi sasa mustakabali wa michuano hiyo
haueleweki.
Sote tunafahamu soka ya Tanzania ni sawa na homa za vipindi
ambazo zinacheza katika kiwango fulani kwa kupanda na kushuka.
Huo ndio, ukweli na hilo linadhihirishwa na takwimu za
viwango vya soka vya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) zinapotoka, Tanzania
inapanda na kuporomoka, haina muendelezo wa kupanda.
Mimi si muumini sana wa takwimu hizi za FIFA, ingawa zina
maana na zinatoa hali halisi, lakini mara nyingine nchi nyingine zinapanda
katika staili ya maji kupwa na maji kujaa.
Katika miaka ya karibuni soka yetu ilipanda hadi tukashika
nafasi ya 89, katika mwezi Desemba mwaka 2007, wakati bado Mbrazil Marcio
Maximo ni kocha mkuu wa timu yetu ya taifa, Taifa Stars.
Kwa sasa
Tanzania ni ya 123, hii ikiwa ni miaka mitatu baadaye tangu tupande hadi ndani ya timu 90
zenye kiwango kizuri cha soka duniani.
Sasa tunalekea wapi? Hilo ndilo swali la kujiuliza ikiwa
matokeo ya karibuni ndio haya tunayoyashuhudia sasa, tumefikia hadi kufungwa na
Timu B ya Afrika Kusini kwenye Uwanja wetu wa nyumbani, kutoka kuwafunga
washiriki wa fainali za Kombe la Dunia New Zealand.
Tatizo letu si makocha na hata kama makocha ni tatizo kweli,
ni vigumu kujua kwa sababu mfumo wetu ndio mbovu na hautoi fursa ya kuwa na
wachezaji bora.
Nchi nyingi za Afrika zinabebwa na nyota wao wanaocheza
Ulaya, lakini sisi tunategemea zaidi wachezaji wa nyumbani na ambao watatoka
kwenye Ligi Kuu tu.
Kutoka kwenye wastani wa wachezaji 450 wanaocheza Ligi Kuu ya
Bara isiyo na ushindani, inayonuka rushwa na uvundo wa uozo wa marefa wetu
wasiojua, manazi na wala hongo ndio tunategemea kupata wachezaji wa kuunda timu
ya taifa.
Rejea msimu uliopita, ligi yenye timu 12 maana yake kila timu
ilicheza mechi 22 na bingwa akapatikana. Katika wachezaji hao 400, inawezekana
nusu yake tu walicheza japo mechi 20 za msimu, wakati kitaalamu ili mchezaji
awe fiti, anatakiwa kucheza mechi zisizopoungua 40 kwa msimu.
TFF pale wana Kurugenzi ya Ufundi, chini ya mwalimu
aliyebobea tu Sunday Burton Kayuni ambaye sina shaka analijua hili, lakini je
ametoa mwongozo utakaotuwezesha kuwa na mfumo bora na amepuuzwa au hajatoa?
Wanajua wenyewe.
Rais mwenyewe wa TFF, Leodegar Chillah Tenga kitaaluma pia ni
kocha na mchezaji mstaafu wa kiwango cha kimataifa, je hayajui haya?
Tanzania tumekuwa watu wa kukariri kariri mambo, wengi sasa
wanasema ‘youth’ na mashindano mengi ya vijana yameanzishwa, lakini je
yanaendeshwa kwa malengo? Hapo kuna shaka.
Klabu za Ligi Kuu zimeshinikizwa kaunzisha timu za vijana na
sasa ni takriban mwaka wa nne, tujiulize vipi kuhusu maendeleo ya timu hizo za
vijana?
Tuna mashindano mengi ya vijana, lakini kutoka kwenye
mashindano hayo mchezaji anaendelezwaje?
Nchi nyingi duniani mbali ya kuwa na Ligi Kuu, zina
mashindano mengine madogo yenye msisimko kama Kombe la Ligi, Kombe la FA na
Super Cup. Pia wana Ligi za vijana madhubuti, mfano pale England ligi ambayo
imemkomaza kiungo chupukizi Mtanzania, Adam Nditi akiwa na Chelsea.
Uganda wana ligi hadi ya wachezaji wa akiba, ambayo
imewasaidia mno kuwafanya wachezaji wao wengi wawe fiti, kwa sababu wasiocheza
katika vikosi vya kwanza vya klabu zao, wanapata changamoto kupitia ligi hiyo.
Hakika mashindano haya yanaongeza msisimko wa soka katika
nchi husika na wakati fulani yanafanya nchi iwe na bingwa zaidi ya mmoja.
Birmingham City ‘The Blues’ ya England waliotaka kuzuru
nchini mwaka jana kucheza na vigogo wa soka hapa nchini, Simba na Yanga, wakati
huo walikuwa ni mabingwa wa Kombe la Ligi, ingawa wamekwishaipa mkono wa
kwaheri Ligi Kuu.
Birmingham waliifunga Arsenal katika fainali ya Kombe la Ligi
mabao 2-1, Mnigeria Obafemi Martins akifunga la ushindi, msimu ambao Manchester
City walitwaa ubingwa wa Kombe la FA na Man United ubingwa wa Ligi Kuu.
Hapa Tanzania, baada ya Ligi Kuu, watu wanasubiri mashindano
ya ujanja ujanja tu ya watu kujitengenezea fedha, lakini hakuna tena mashindano
mengine makubwa, zaidi ya hiyo michuano ya BancABC Sup8R iliyoanza mwaka huu na
Simba B ikatwaa ubingwa.
Faida ya mashindano ya ziada kama Kombe la FA ni kutoa fursa
kwa wachezaji ambao hawana namba kwenye vikosi vya kwanza nao kucheza. Kwa
mfano, Kombe la FA tutarajie hadi Friends Rangers ya Manzese na Ugimbi ya
Kurasini zitacheza, maana yake sasa klabu za Ligi Kuu zitaweza kutumia
wachezaji wake wa vikosi vya pili, jambo ambalo litasaidia kuwakomaza.
Wakati umefika sasa, TFF ifunguke zaidi na kupanua wigo wa miundombinu
ya kuinua soka ya nchi hii badala ya kuishia kufikiria tu kuwa na mashindano ya
mpito pekee. Tunahitaji michuano zaidi ambayo mchezaji atacheza mechi zaidi ya
10 akionyesha umahiri ule ule.
Mifano ipo, wachezaji kama Abuu Ramadhan ‘Amokachi’,
aliyewahi kucheza Yanga kabla ya mizengwe kumuondoa kwenye soka angali mdogo,
alitokea kwenye mashindano ya Kombe la FA wakati bado yanafanyika nchini,
akiichezea Baker Rangers ya Magomeni.
Ukweli ni kwamba Tanzania bado tuna safari ndefu kuelekea
kwenye mafanikio na maana yake kazi kubwa inahitaji kufanyika, lakini ajabu TFF
wanaonekana kuridhishwa na hali iliyopo.
Tazama sasa Kombe la Taifa limekufa kifo cha kawaida,
kutokana na kile ambacho sisiti kusema TFF kuzidiwa ujanja au kutokuwa na
mitazamo ya mbali.
Kombe la Taifa limekufa kwa sababu ya kukosa udhamini- baada
ya mdhamini wake wa awali, Kampuni Bia
Tanzania (TBL) iliyokuwa ikidhamini michuano hiyo kupitia bia ya
Kilimanjaro Premium Lager kuachia michuano hiyo.
Wazi, TBL walijitoa Taifa Cup baada ya kupata dili la
kujitangaza kupitia timu ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ambayo awali
ilikuwa inadhaminiwa na kampuni nyingine ya Bia nchini, Serengeti (SBL).
Mkataba wa udhamini wa Taifa Stars na SBL ulimalizika Desemba
mwaka jana na TFF ikashindwa kukubaliana dau la mkataba mpya na SBL, na kuingia
mkataba mpya naTBL. TFF waliuita mkataba huo ni mnono sana. Kweli kabisa, kwa
sababu TBL walipanda dau, kutoka lile walilokuwa wakitoa SBL.
SBL walianza kuidhamini Stars mwaka 2006, ikiwa haina na
haijawahi kuwa na mdhamini. Katika kipindi hicho, SBL ilitekeleza vema mkataba
wake wa udhamini na timu hiyo na kuonekana dhahiri kuvuka mipaka katika
kuhakikisha timu inakuwa na maandalizi mazuri na kujenga hamasa ya mashabiki kurejesha
mapenzi kwa timu yao ya taifa.
TFF walishindwa kusoma ishara za nyakati wakaingia kichwa
kichwa kwa TBL na kuwapa mkataba wa
kudhamini timu ya taifa, hawakujua nini kitatokea mbele. TBL ipo kibiashara
zaidi na daima wataendelea kuangalia maslahi yao zaidi juu ya kile wanachotoa,
kama kitaendana na wanachopata- sijui TFF wanafikiria nini, lakini matokeo yake
ndiyo haya, Kombe la Taifa ‘marehemu’.
Sasa basi, TFF watuambie na kuhusu Kombe la FA kama ilikuwa ‘magumashi’
tujue, maana tumezoea usanii huu katika soka yetu. Ndiyo, watuambie tujue na
ili tujue zaidi soka yetu inapoelekea. Jumatano njema.