Tenga katikati akizungumza na Waandishi leo. Kulia ni Sunday Kayuni na kushoto Angetile Osiah |
Na Prince Akbar
RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania
(TFF), Leodegar Tenga amezitaka Kamati za Uchaguzi kufanya kazi kwa kuzingatia
Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF ili kuwa na uchaguzi huru na wa haki.
Akizungumza na Waandishi wa Habari,
Dar es Salaam leo, makao makuu ya TFF, Ilala, Dar es Salaam, Tenga ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), amesema
uongozi wa mpira wa miguu unahitaji uamuzi mgumu, hivyo Kamati za Uchaguzi
ambazo zimeundwa kwa mujibu wa Katiba zinatakiwa kufanya kazi kwa kuzingatia
kanuni na si kuangalia sura za watu.
Amepongeza kamati zilizosimamia
uchaguzi kwa kufuata kanuni, na ingawa kila mtu ana haki ya kuongoza, jambo
lolote lazima liwe na kanuni, kwani hata kwenye mikutano ya hadhara kuna
kanuni.
“Huwezi kufika kwenye mkutano wa
hadhara na wewe unaanzisha mkutano wako. Lazima kanuni ziheshimiwe ili kufanya
uchaguzi uwe huru na wa haki. Nini kimetokea kwenye maeneo ambayo kuna
matatizo? Kila mwanachama wetu (mkoa/chama shiriki) ana Kamati ya Uchaguzi
ambayo imeundwa kwa mujibu wa kanuni.
“Zile kamati hazitekelezi majukumu
yake, unampitisha mtu unajua hana sifa unasema acha akafie mbele (Kamati ya
Uchaguzi ya TFF). Kanuni zinasema jaza fomu mwenyewe, weka nakala za vyeti na
si kwamba huyu tunamjua. Kanuni zinatakiwa zifuatwe, ukienda kinyume
unaondolewa,” amesema.
Amesisitiza kamati zifanye kazi kwa
kufuata kanuni ili kusaidia mpira wa miguu kwani zimeundwa kihalali, kwa hiyo
zisiogope kuengua hata walioziteua kama hawana sifa.
Pia Rais Tenga amezitaka Kamati za
Utendaji na Sekretarieti kutoziingilia Kamati za Uchaguzi katika mchakato wa
uchaguzi, badala yake zinatakiwa kuziwezesha tu (facilitation).
Amesema baadhi ya wagombea nao ni
tatizo kwani wanaingia kwenye uchaguzi bila kuzielewa Katiba za vyama vyao na
Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, hivyo ni vizuri wakazielewa kwanza.
Rais Tenga amesema ni vizuri
wanachama wote wakafanya uchaguzi kabla ya uchaguzi wa TFF utakaofanyika
Desemba mwaka huu ili wapate fursa ya kupiga kura kwenye uchaguzi huo wa
shirikisho.
Amewataka pia wadau kujitokeza kwa
wingi kuwania uongozi kwenye chaguzi za vyama wanachama wa TFF, kwani mwitikio
umeonekana kuwa mdogo kulinganisha na umaarufu wa mchezo wenyewe.
Amepongeza vyama vya mikoa ambavyo
tayari vimefanya uchaguzi wao. Baadhi ya vyama hivyo ni Arusha, Dodoma, Iringa,
Kagera, Kigoma, Kilimanjaro, Manyara, Mara, Morogoro, Mtwara na Singida.