Rais wa ^TFF, Leodegar Chilla Tenga (katikati) akizungumza na Waandishi wa Habari. Kulia kwake ni Sunday Burton Kayuni, Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF na kushoto Katibu, Angetile Osiah Malabeja. |
Na Mahmoud Zubeiry
RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chillah
Tenga amesema kwamba kwa sasa shirikisho lake linawaachia wadhamini wa Ligi
Kuu, Vodacom watumie busara kumalizana na klabu ya Yanga, juu ya mgogoro wao
kuhusu nembo ya ligi hiyo.
Akijibu swali la BIN ZUBEIRY katika Mkutano wake
maalum na Waandishi wa Habari leo makao makuu ya TFF, kuzungumzia masuala ya
uchaguzi wa vyama mbalimbali vya soka nchini, Tenga alisema kwamba kwa kuwa
msimu uliopita Vodacom walimalizana na Yanga bila kulishirikisha shirikisho
lake, na mwaka huu wanawaachia pia.
“Kitendo kilichofanywa na Vodacom mwaka jana, kumalizana na
Yanga bila kutushirikisha kuhusu utata wa nembo, sisi tulijua kitaleta matatizo
baadaye, na kweli sasa yametokea, na ndiyo maana unaweza kuona, sekretarieti
yetu inalipeleka taratibu hili suala,”alisema Tenga.
Tenga alisema Vodacom ingewaacha TFF msimu uliopita
wakaihukumu Yanga kwa mujibu wa kanuni, hata msimu huu ingekuwa rahisi kwao
kuingilia, lakini kwa kuwa msimu uliopita waliingilia na wakaibadilishia klabu
hiyo nembo, basi na msimu huu pia wanawaachia wamalizane wenyewe.
Mwaka jana Yanga waligoma kuvaa jezi zenye nembo ya wadhamini
wa Ligi Kuu, Vodacom kwa sababu zina nembo nyekundu hadi kampuni hiyo
ikawabadilishia na kuwapa jezi maalum zenye nembo nyeusi.
Mwaka huu pia, Yanga wamekataa kubandikiwa nembo za Vodacom
kwenye jezi zao kwa sababu ya rangi hiyo nyekundu na jana wamecheza mechi ya
sita bila kuvaa nembo ya mdhamini, wakisistiza wabadilishiwe.
Wakati huo huo, kanuni za Ligi Kuu zinasema timu itakayogoma
kuvaa nembo ya mdhamini itashushwa Daraja, ingawa tishio hilo la kanuni sasa
linapozwa na kauli ya Tenga leo.