Na Mahmoud Zubeiry
RAIS wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Leodegar Chillah
Tenga amesema kwamba vita dhidi ya rushwa katika Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara ni ngumu na inahitaji sapoti kubwa ya wadau na wapenzi wa mchezo wenyewe
ili kuifanikisha.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo, makao makuu ya TFF,
Ilala mjini Dar es Salaam, Tenga alisema kwamba pamoja awali kuwepo kwa
mazingira ya ushahidi wa rushwa, lakini wanashindwa kwa sababu wao wana mipaka
yao.
“Hili la rushwa kwa kweli ni gumu, ni gumu kwa sababu sisi
tuna mipaka yetu, lazima tupate ushirikiano na vyombo husika. Lazima tupate ushirikiano
wa wapenzi wenyewe wa mpira,”alisema Tenga.
Beki huyo wa zamani wa kimataifa wa Tanzania, alisema wakati
mwingine inakuwa vita hiyo inakuwa ngumu zaidi anaposikia hata Waandishi wa
Habari wanahusika.
“Mimi sijathibitisha, lakini watu wananiambia viongozi
wenyewe wanashiriki mchezo huu. Tena nasikia hadi nyinyi Waandishi wa Habari
wakati mwingine mnatumiwa kupenyeza rushwa, kwa kweli inasikitisha,”alisema
Tenga.
Kuhusu vipimo vya dawa za kulevya katika Ligi Kuu, Tenga
alisema kwamba mchakato wa zoezi hilo unaendelea na walichokifanya kwa sasa ni
kuwataaribu na kuwapa muda wahusika waache taratibu.
Alisema wamewapa nusu msimu watumiaji wa mihadarati katika
soka ya Tanzania kujiondoa taratibu na tayari wamekwishawaambia hadi viongozi wa klabu zote, ili zoezi hilo likianza
liende vizuri.
“Hatutaki kuwaadhiri vijana wetu, ndiyo maana tumewaambia mapema,
ili wale ambao wanavuta bangi kwa mfano, waanze taratibu kula chwingamu waache
bangi, ili wakati utakapofika, hakutokuwa na mzaha,”alisema Tenga.