Magesa |
Na Princess Asia
MASHINDANO ya mpira wa Kikapu ya kombe la Taifa, yanatarajiwa
kufanyika mjini Tanga kuanzia Oktoba 29 hadi Novemba 4, mwaka huu.
Makamu wa rais wa Shirikisho la Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF),
Phares Magesa ameiambia BIN ZUBEIRY leo kwamba, mashindano
haya ya Kombe la Taifa kwa kawaida ndio hutumika kuchagua timu zetu za Taifa,
hvyo ni muhimu kwa mikoa yote kushiriki ili kuwapa nafasi wanamichezo kutoka
mikoa yao kuonekana katika ngazi ya Taifa.
Ameitaja mikoa iliyothibitisha hadi sasa ni Iringa, Mbeya,
Arusha, Kilimanjaro, Shinyanga, Singida, Mara, Dodoma, Pemba, Unguja, Tanga,
Mtwara, Lindi na Dar Es Salaam.
“Bado nafasi ya kuthibitisha kushiriki ipo kwa wanaopenda
kushiriki katika mashindano haya na ratiba ya mashindano itapangwa tarehe
28/10/2012 katika kikao ambacho wawakilishi wa mikoa yote lazima wawepo na ndo
itakuwa mwisho wa kuthibitisha kushiriki,”alisema.
Akizungumzia makocha wa timu yaifa kutoka Marekani, Magesa alisema
Kocha Mkuu atakuwa Albert Sokaitis mwenye uzoefu wa miaka 24, ambaye kwa sasa anafundisha
timu ya Chuo Kikuu cha Post, Marekani katika jimbo la Connecticut, ambaye pia
amewahi kufundisha timu na kuendesha mafunzo nchi za Uchina, Lebanon, Ugiriki
na Japan.
Amesema Sokaitis atasaidiwa na Jocquis L. Sconiers mwenye
uzoefu wa miaka mingi, ambaye kwa sasa ni Kocha Msaidizi wa timu ya Chuo Kikuu
cha Post huko Marekani katika jimbo la Connecticut.
“Walimu wote hawa wana shahada za juu kutoka vyuo vikuu mbali mbali vya Marekani na katika
utekelezaji wa mpango huo katika awamu ya kwanza Kocha Sconiers anatarajiwa
kuwasili nchini Oktoba 30 na ataelekea
Tanga siku inayofuata katika Kombe la Taifa ili kuchagua wachezaji wa timu za taifa
(wanawake na wanaume) na baada ya hapo ataanza kazi rasmi kwa timu zote Novemba
5,”alisema.
Alisema awamu hii ya kwanza ya mpango wa mafunzo unadhaminiwa
na watu wa Marekani kupitia ubalozi wao hapa Tanzania na kwamba wanawashukuru kwa
msaada huo.
Aidha, Magesa alisema kama mipango yote ikienda vizuri, wanatarajia
kuwa wenyeji wa mashindano ya kanda ya Tano ya FIBA, yanayotarajiwa kufanyika mjini
Dar es Salaam kuanzia Desemba 15 hadi 22, mwaka huu.
“Hivyo basi Kocha huyo atatumia nafasi hii kuanza maandalizi
ya timu zetu za Taifa kuziandaa kwa mashindano haya yanayotarajiwa kushirikisha
nchi za Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Ethiopia, Eritrea, Somalia,
Djibouti, Misri Sudan na Sudani ya kusini,”alisema.
Kuhusu Mkutano Mkuu wa TBF, alisema wanatarajia utafanyika Novemba
1 hadi 2, mwaka huu na amewataka viongozi wote wa Mikoa na wawakilishi
wachezaji, vyama shiriki kushiriki bila kukosa katika mkutano huu utakaofanyika
Tanga.