Salum Abubakar 'Sure Boy Jr.' |
Na Mahmoud Zubeiry
KIUNGO bora Afrika Mashariki kwa
sasa, Salum Abubakar ‘Sure Boy Jr.’ amepona kabisa na ameongozana na kikosi cha
klabu yake Azam FC kilichokwenda Morogoro, kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara dhidi ya wenyeji Polisi kesho kwenye Uwanja wa Jamhuri,
Morogoro.
Sure amekuwa majeruhi kwa muda
mrefu na msimu tangu uanze alijaribu kuingizwa kwenye mechi tatu, lakini
akashindwa kucheza vema kutokana na maumivu, aliyoyapata kwenye michuano ya
Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Julai mwaka huu.
Aliingia akitokea benchi kwenye
mechi ya Ngao ya Jamii dhidi ya Simba, ambayo Azam ililala 3-2 na akaingia tena
kwenye mechi na JKT Ruvu ambayo Azam ilishinda 3-0 na mechi iliyopita dhidi ya
African Lyon, ambayo Azam ilishinda 1-0, Sure aliingia tena akitokea benchi.
Kama ataanza kwenye mechi ya kesho
na Polisi, hiyo itakuwa ya kwanza kwake tangu kuanza kwa Ligi Kuu na kulingana
na maendeleo ya afya yake, kuna uwezekano mkubwa kesho kocha Mserbia, Boris
Bunjak akamuanzisha mtoto huyo wa winga wa zamani wa Yanga, Abubakar Salum
‘Sure Boy’.
Azam jana walifanya mazoezi kwenye
Uwanja wa Chamazi asubuhi na jioni wakapanda basi lao, lenye kila kitu ndani-
TV, friji, choo, mziki wa maana na siti za kulala kwa safari ya takriban saa
mbili kwenda Mji Kasoro Bahari, Morogoro.
Azam imepania kushinda mechi hiyo
Jumamosi ili kuiondoa Simba kileleni na kuzidi kuweka hai matumaini ya kutwaa
ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu.
Katika kujiandaa na mechi ya
Morogoro, Azam Jumanne ilicheza mechi ya kujipima nguvu na kufungwa na Simba SC
mabao 3-2 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika asubuhi kwenye Uwanja wa
Chamazi, maarufu kama Azam Complex, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Mabao ya Simba siku hiyo yalifungwa
Ramadhani Singano ‘Messi’, Uhuru Suleiman ‘Robinho’ na Daniel Akuffo, wakati ya
Azam yalifungwa na Jamil Mchauru na Khamis Mcha.
Hiyo ilikuwa mechi ya nne Azam
inafungwa na Simba msimu huu katika mechi tano walizokutana hadi sasa, baada ya
awali kufungwa kwa penalti kwenye fainali ya Kombe la Urafiki, kufuatia sare ya
2-2, kufungwa 2-1 kwenye Nusu Fainali ya BancABC Sup8R na 3-2 kwenye mechi ya
Ngao ya Jamii, wakati wao walishinda 3-1 dhidi ya Wekundu hao wa Msimbazi,
katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame.
Azam na Simba zitakutana tena
katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara, mzunguko wa kwanza, Oktoba
27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba ndio inaongoza Ligi Kuu, hadi
sasa ikiwa imeshinda mechi tano kati ya sita ilizocheza na moja tu imetoka
sare, hivyo kujikusanyia pointi 16, wakati Azam inashika nafasi ya pili
ikizidiwa pointi tatu, ingawa pia iko nyuma kwa mchezo mmoja.
Mbali na Sure, wachezaji wengine wa
Azam ambao bado majeruhi ni Waziri Salum, Ibrahim Jeba, wakati Samir Haji Nuhu
anatumikia adhabu ya kadi hajaenda pia Morogoro sawa na Jackson Wandwi na
Hamisi Mcha ‘Vialli’, ambao hawamo kabisa kwenye mipango ya kocha katika mechi
hiyo.