Bunjak |
Na Mahmoud Zubeiry
WACHEZAJI wa
Azam ndio waliomponza kocha Mserbia, Boris Bunjak kufukuzwa kazi jana, baada ya
kuuandikia barua uongozi, wakisema hawaridhishwi na ufundishaji wa kcoha huyo
na hawamtaki.
Pamoja na
kumchongea kwa uongozi Mserbia huyo, habari za ndani kutoka Azam zimesema kwamba,
ni wachezaji hao hao waliopendekeza katika barua yao kurejeshwa kwa aliyekuwa
kocha wa timu hiyo, Muingereza Stewart Hall.
Habari zilizopatikana
jana kutoka Azam FC, zilisema kwamba, sababu za kufukuzwa kwa Mserbia huyo ni
kushuka kwa kiwango cha timu, hali iliyosababisha sasa ianguke hadi nafasi ya
nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Tayari
Bunjak amekwishapewa haki zake zote na ataondoka kesho, siku ambayo Stewart anaweza
kuwasili kuanza tena kazi Azam FC.
Bunjak
anaondoka Azam baada ya kuiongoza timu katika mechi 16, akifungwa nne tu, zote
dhidi ya Simba ikiwemo ya juzi ya Ligi Kuu, waliyofungwa 3-1 na kutoa sare
tatu.
Bunjak
mwenye leseni ya Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), alitua Azam, Agosti 7, mwaka
huu akitokea FC Damac ya Saudia Arabia aliyoanza kuifundisha mwaka jana na
kabla ya hapo alifundisha klabu kibao za kwao, zikiwemo FK Sloga Kraljevo, FK
Javor Ivanjica, Crvena Zvezda Gnjilane, FK Radnicki Nis, FC Uralan Elista, FK
Mladi Radnik, FK Crvena Zvezda Beograd, Al-Shaab, FK Hajduk Kula na Al-Nasr.
Awali,
Bunjak aliyezaliwa Novemba 17, mwaka 1954 ( miaka 57), alicheza soka katika
klabu za FK Sloga (Kraljevo), FK Vozdovac (Beograd), FK Radnicki (Kragujevac),
FK Olimpia (Ljubljana), FK Sumadija (Arandjelovac), FK Sloga (Kraljevo), FK
Borac (Cacak) na FK Sloga (Kraljevo).
Stewart
alifukuzwa kwa kosa la kukaidi maagizo ya Bodi ya Ukurugenzi ya klabu hiyo,
kumpanga Mrisho Khalfan Ngassa katika mechi ya fainali ya Klabu Bingwa Afrika
Mashariki na Kati, Kombe la Kagame dhidi ya Yanga.
Mserbia huyo
anakuwa kocha wa tano kufukuzwa Azam, ndani ya miaka minne tangu ianze kucheza
Ligi Kuu, 2008 baada ya Stewart, Mbrazil Neider dos Santos, Sylvester Marsh na
Itamar Amorin, Mbrazil mwingine.
Lakini Stewart
angalau aliacha kumbukumbu ya taji na Medali Azam, baada ya kuiwezesha kutwaa
Kombe la Mapinduzi Januari, kushika nafasi ya pili katika Ligi Kuu Aprili,
kabla ya kushika nafasi ya pili Kombe la Urafiki na Kagame mwezi uliopita,
mambo ambayo bila shaka yamemfanya afikiriwe tena.
Stewart ana
sifa ya kutokuwa mbinafsi na mwenye kuwaamini watu wa chini yake, kwa mfano
namna ambavyo alikuwa akimpromoti Kali Ongala. Alimkuta Kali kama mchezaji,
lakini kwa sababu ya umri kumtupa mkono, akashauriana naye awe Kocha Msaidizi
na mshambuliaji huyo wa zamani wa Yanga, akakubali.
Chini ya
Stewart, Kali alikuwa akiachiwa timu aiongoze ili kumjengea kujiamini zaidi na
mwezi uliopita aliachiwa timu kwenye Kombe la Urafiki, akaifikisha fainali,
ambako ilifungwa na Simba kwa penalti kufuatia sare ya 2-2 ndani ya dakika
90.
REKODI YA BORIS BUNJAK AZAM
Azam 2-1
Polisi (BancABC)
Azam 1-2
Simba B (BancABC)
Azam 8-0
Trans Camp (Kirafiki)
Azam 1-0
Prisons (Kirafiki)
Azam 2-0
Coastal Union (Kirafiki)
Azam 2-3
Simba SC (Ngao ya Jamii)
Azam 1-0
Kagera Sugar (Ligi Kuu)
Azam 2-2
Toto African (Ligi Kuu)
Azam 3-0 JKT
Ruvu (Ligi
Kuu)
Azam 1-0
Mtibwa Sugar (Ligi Kuu)
Azam 1-0
African Lyon (Ligi Kuu)
Azam 2-3
Simba SC (Kirafiki)
Azam 1-0
Polisi (Ligi Kuu)
Azam 0-0 Prisons (Ligi Kuu)
Azam 1-1
Ruvu Shooting (Ligi Kuu)
Azam 1-3
Simba (Ligi Kuu)