Simba SC |
Na Princess Asia, aliyekuwa Tanga
SIMBA SC imerejea Dar es Salaam leo mchana na inatarajiwa
kuingia kambini moja kwa moja kuanza maandalizi ya mechi ijayo ya Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, dhidi ya Azam FC, Oktoba 27, mwaka huu, Uwanja wa Taifa,
Dar es Salaam.
Simba SC itakuwa na wiki nzima ya kujiandaa na mechi hiyo,
ikitoka kulazimishwa sare ya tatu mfululizo jana kwenye Uwanja wa Mkwakwani
mjini Tanga, baada ya kutoka 0-0 na wenyeji Mgambo Shooting katika mfululizo wa
Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Matokeo hayo, yanaifanya Simba ifikishe pointi 19, baada ya
kucheza mechi tisa na kuendelea kuongoza Ligi Kuu, ingawa wameuweka rehani
usukani wa ligi hiyo kwa Azam ambayo Jumatano inacheza na Ruvu Shooting Uwanja
wa Chamazi, Dar es Salaam.
Awali ya hapo, Simba ilitoka 2-2 na Kagera Sugar Uwanja wa Taifa
na 0-0 na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani.
Azam yenye pointi 17, ikishinda itafikisha pointi 20 na
kupanda kileleni, tena ikiwa nyuma kwa mchezo mmoja, kwani hadi sasa imecheza
mechi saba. Yanga iliyocheza mechi nane, ina pointi 14 katika nafasi ya tatu
nayo itacheza na Polisi Morogoro keshokutwa.
Katika mechi ya jana ya Simba na Mgambo, iliyochezeshwa na refa
Athumani Lazi wa Morogoro, dakika 45 za kwanza, timu zote zilishambuliana kwa
zamu na zilionyesha kiwango kizuri, ushindani mkubwa- kwa ujumla ilikuwa
burudani.
Kipindi cha pili kadhalika pamoja na kocha Mserbia, Profesa
Milovan Cirkovick kufanya mabadiliko akiwatoa Mrisho Ngassa na Amri Kiemba na
kuwaingiza Edward Christopher na Salim Kinje, bado walishindwa kuifunga Mgambo
iliyopanda Ligi Kuu msimu.
Katika dakika 10 za mwisho, ilishuhudiwa Mgambo wakicheza kwa
kujihami zaidi kutokana na presha kali ya mashambulizi ya Simba SC.
Katika mechi hiyo, kikosi cha Mgambo kilikuwa; Godson Mmasa,
Yassin Awadh, Salum Mlima, Bakari Mtama, Salum Kipanga, Ramadhani Malima,
Chande Magoja/Nassor Gumbo dk85, Mussa Ngunda, Issa Kandulu, Fully Mganga na
Juma Mwinyimvua.
Simba SC;Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah,
Hassan Hatibu, Paschal Ochieng, Jonas Mkude, Amri Kiemba/Salim Kinje dk88,
Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Emmanuel Okwi na Mrisho Ngassa/Edward Christopher
dk 79.