Wachezaji wa Simba SC |
Na Mahmoud Zubeiry
SIMBA SC tangu inaondoka leo Dar es Salaam kwenda Morogoro
tayari kwa mchezo wao dhidi ya Polisi mjini Morogoro katika mfululizo wa Ligi
Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kesho, wakitoka kushinda mabao 3-1 dhidi ya Azam
FC Jumamosi na kujiimarisha kileleni.
Mabingwa hao watetezi juzi na jana walifanya mazoezi kwenye
Uwanja wa Kinesi, Urafiki, Manzese, Dar es Salaam na kwa ujumla timu vizuri
kuelekea mchezo huo wa tatu kucheza nje ya Uwanja wa Taifa, msimu huu baada ya
awali kucheza mechi mbili Tanga dhidi ya Coastal Union na Mgambo JKT ambazo
zote walilazimishwa sare ya bila kufungana.
Simba imeshinda mechi zake zote Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam na kutoa sare mbili tu, dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga 1-1 na 2-2
dhidi ya Kagera Sugar ya Bukoba.
Wekundu hao wa Msimbazi, wapo kileleni mwa Ligi Kuu kwa
pointi zao 22 baada ya kucheza mechi 10, wakifuatiwa na wapinzani wao wa tangu
enzi za bibi na babu, Yanga SC wenye pointi 20 katika nafasi ya pili.
Beki Juma Said Nyosso na kiungo Haruna Moshi Shaaban ‘Boban’
wanaendelea kutumikia adhabu zao za kusimamishwa, lakini wachezaji wote wengine
wapo fiti kabisa, ukiondoa Obadia Mungusa aliyefukuzwa mapema tu kabla ya
kuanza kwa Ligi Kuu.
Simba itamenyana na Polisi iliyorejea Ligi Kuu msimu huu, ambayo
inashika mkia katika ligi hiyo, ikiwa haijashinda hata mechi moja tangu kuanza
kwa ligi hiyo zaidi ya kutoa sare mbili.
Lakini hiyo haiifanyia Simba idharau mechi hiyo na kocha
Mserbia, Milovan Cirkovick ameanza maandalizi ya mapema kwa ajili ya mechi
hiyo.
Hofu kubwa kwa Simba ni hali ya Uwanja wa Jamhuri, Morogoro-
ni mbaya na kulingana na uzoefu walioupata wa kucheza kwenye Uwanja mwingine
mbovu wa Mkwakwani, Tanga wanajua watakuwa na shughuli pevu keshokutwa.
Hadi sasa Simba ndio timu pekee katika Ligi Kuu, ambayo
haijapoteza mechi, ikiwa imeshinda mechi sita na kutoa sare nne, wakati Yanga
imefungwa mechi mbili na Azam FC na Coastal Union zinazoifukuzia timu hiyo, zimefungwa
mechi moja moja.