Wachezaji wa Simba |
Na Princess Asia
SIMBA SC imefanya mazoezi kwenye ufukwe wa Coco leo asubuhi
na wachezaji wote wameruhusiwa kurudi manyumbani kwao, kujiandaa kwa safari ya
Zanzibar jioni kwenda kuweka kambi ya kujiandaa na mechi dhidi ya Azam FC
Jumamosi wiki hii Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa kawaida Simba SC huenda Zanzibar katikati ya Ligi Kuu
kuweka kambi linapokaribia pambano dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC
lakini kwa kitendo cha kwenda kujichimbia huko kwa ajili ya Azam, maana yake
wanaipa uzito huo mechi hiyo.
Kikosi cha Simba kilirejea Dar es Salaam jana mchana kutoka
Tanga ambako kilitoka sare ya bila kufungana na wenyeji Mgambo JKT Jumapili
katika mfululizo wa ligi hiyo.
Matokeo hayo, yanaifanya Simba ifikishe pointi 19, baada ya
kucheza mechi tisa na kuendelea kuongoza Ligi Kuu, ingawa wameuweka rehani
usukani wa ligi hiyo kwa Azam ambayo kesho inacheza na Ruvu Shooting Uwanja wa
Chamazi, Dar es Salaam.
Awali ya hapo, Simba ilitoka 2-2 na Kagera Sugar Uwanja wa
Taifa na 0-0 na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani.
Azam yenye pointi 17, ikishinda itafikisha pointi 20 na
kupanda kileleni, tena ikiwa nyuma kwa mchezo mmoja, kwani hadi sasa imecheza
mechi saba. Yanga iliyocheza mechi nane, ina pointi 14 katika nafasi ya tatu
nayo itacheza na Polisi Morogoro keshokutwa.
Baada ya sare ya Jumapili, Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj
Ismail Aden Rage amewataka wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kuwa watulivu na
wasikatishwe na tamaa na sare tatu mfululizo za timu hiyo katika Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, kwani safari bado ni ndefu.
Rage amesema kwamba, hadi sasa timu yao haijafungwa katika
Ligi Kuu kuashiria kwamba bado ni timu bora na matokeo ya sare hizo tatu
mfululizo pia ni kutokana na uimara wa timu yao.
Rage ameonya wanachama wenye desturi ya kutoa maneno ya
uchochezi timu inapoyumba kidogo, waache kufanya hivyo kwa sababu wanaweza kuvuruga
amani iliyopo sasa klabuni.