Kikosi cha Simba |
Na Princess Asia
WEKUNDU wa Msimbazi, Simba SC wanatarajiwa kurejea kesho Dar
es Salaam wakitokea Zanzibar ambako waliweka kambi ya wiki moja kujiandaa na
mchezo wa kesho wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara dhidi ya Azam FC, Uwanja wa
Taifa.
Pamoja na Juma Nyosso na Haruna Moshi kusimamishwa, lakini
wachezaji waliobaki wana morali ya hali ya juu na wamepania kushinda mechi ya
kwanza kati ya nne, baada ya sare tatu mfululizo.
Kwa kawaida Simba SC huenda Zanzibar katikati ya Ligi Kuu
kuweka kambi linapokaribia pambano dhidi ya mahasimu wao wa jadi, Yanga SC
lakini kwa kitendo cha kwenda kujichimbia huko kwa ajili ya Azam, maana yake
wanaipa uzito huo mechi hiyo.
Simba ilienda Zanzibar Jumanne, siku moja baada ya kurejea
kutoka Tanga, ambako ililazimishwa sare ya bila kufungana na wenyeji Mgambo JKT
Jumapili katika mfululizo wa ligi hiyo.
Matokeo hayo, yaliifanya Simba ifikishe pointi 19, baada ya
kucheza mechi tisa na kuendelea kuongoza Ligi Kuu.
Awali ya hapo, Simba ilitoka 2-2 na Kagera Sugar Uwanja wa
Taifa na 0-0 na Coastal Union Uwanja wa Mkwakwani.
Baada ya sare ya Jumapili, Mwenyekiti wa Simba SC, Alhaj
Ismail Aden Rage amewataka wanachama na wapenzi wa klabu hiyo kuwa watulivu na
wasikatishwe na tamaa na sare tatu mfululizo za timu hiyo katika Ligi Kuu ya
Vodacom Tanzania Bara, kwani safari bado ni ndefu.
Rage amesema kwamba, hadi sasa timu yao haijafungwa katika
Ligi Kuu kuashiria kwamba bado ni timu bora na matokeo ya sare hizo tatu
mfululizo pia ni kutokana na uimara wa timu yao.
Rage ameonya wanachama wenye desturi ya kutoa maneno ya
uchochezi timu inapoyumba kidogo, waache kufanya hivyo kwa sababu wanaweza
kuvuruga amani iliyopo sasa klabuni.