Juma Nyosso |
Na Prince Akbar
SIMBA SC inamsubiri kwa hamu beki wake Juma Said Nyosso na
pendekezo lake la kuvunja mkataba na klabu hiyo, lakini itamkata maini na jibu
moja tu.
Jibu gani hilo? Atatakiwa kuilipa klabu hiyo fedha za kuvunja
mkataba.
“Sheria ziko wazi na mkataba wake uko wazi, kabla ya kuusaini
aliusoma vizuri, akauelewa akasaini, kwa kuwa yeye ameamua kuvunja mkataba,
basi atatakiwa kutulipa fedha za kuvunja mkataba,”alisema kiongozi mmoja wa
Simba ambaye hakutaka kutajwa jina gazetini.
Kimsingi Simba imekubali kuvunja mkataba na beki wake huyo
iliyedumu naye tangu mwaka 2007, kulingana na maombi yake, na imemtaka afike
kwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili, Zacharia Hans Poppe kujadili suala hilo.
Habari za ndani kutoka Simba SC, zimesema kwamba Nyosso
amewasilisha maombi ya kuvunja mkataba na klabu hiyo, baada ya kushushwa kikosi
cha pili, akidaiwa kiwango chake kimeshuka hivyo amepewa fursa ya kwenda
kukiboresha.
Lakini Nyosso mwenyewe ameona kama hastahili kushushwa timu
ya pili na ameomba asitishiwe mkataba wake aondoke, jambo ambalo uongozi wa
klabu umelikubali.
Nyosso si kama anatuhumiwa kuhujumu timu, bali anaambiwa
uwezo wake umeshuka mno na kwamba amekuwa akiigharimu timu katika siku za
karibuni, hivyo amepewa fursa ya kwenda kupandisha kiwango chake.
Adhabu kama hii amewahi kupewa mshambuliaji wa kimataifa wa
Argentina, Carlos Tevez katika klabu ya Manchester City ya England msimu
uliopita na aliitumikia vizuri hadi aliporejeshwa tena kikosi cha kwanza,
ambako aliisaidia timu kumalizia msimu vizuri kwa kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu.
Mbali na Nyosso, kiungo Haruna Moshi Shaaban amesimamishwa
kwa wiki tatu kwa tuhuma za utovu wa nidhamu na katika kipindi hicho atakuwa
akipokea nusu mshahara.
Boban ameamua kurudi nyumbani kwake kupumzika na mkewe hadi
adhabu hiyo iishe ajue mustakabali wake, ila amesema anaonewa kwa sababu
hakupewa nafasi ya kujibu tuhuma zake kabla ya hatua kuchukuliwa, ingawa
amechukulia poa tu.
Wakati huo huo, habari zaidi kutoka ndani ya Simba, zimesema
kwamba Mwinyi Kazimoto Mwitula, Ramadhan Suleiman Chombo na Mrisho Khalfan
Ngassa nao wanaangaliwa kwa ‘jicho la tatu’ juu ya mwenendo wao kwenye timu
hiyo na kwa nyakati tofauti wote wamekwishaitwa kuhojiwa masuala
mbalimbali.