Simba SC |
Na Mahmoud Zubeiry
MABINGWA watetezi, Simba SC tayari wako mjini Tanga tangu
jana jioni kwa ajili ya mechi yao ya kesho dhidi ya wenyeji JKT Mgambo katika
mfululizo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara.
Simba iliyoanza Ligi Kuu kwa kishindo, ikishinda mechi sita
mfululizo, imelazimishwa sare katika mbili mfululizo zilizopita 0-0 na Coastal
Union mjini Tanga na 2-2 na Kegara Sugar mjini Dar es Salaam na kesho imepania
kumaliza mduduwa sare.
Kocha Mserbia, Profesa Milovan Cirkovick amesema yeye na
wachezaji wake wamejifunza jambo baada ya sare ya pili na Kagera Jumatano na
sasa wataongeza juhudi zaidi ili kuhakikisha matokeo hayo hayajirudii.
Lakini Mgambo nayo, iliyoanza Ligi kizembe, imezinduka na
kushinda mechi tatu mfululizo, tena moja ya ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar 2-1
wiki iliyopita kabla ya kushinda 2-0 dhidi ya Toto African mjini Tanga.
Simba imeenda Tanga na wachezaji wake 24, ambao ni makipa; Juma
Kaseja Juma, Wilbert Mweta William na Waziri Hamad Mwinyiamani, mabeki Nassor
Said Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah Mrisho, Paulo George Ngalema, Koman Bili
Keita, Pascal Ochieng Akullo, Hassan Hatibu Kondo.
Viungo ni Jonas Mkude Gerrald, Ramadhani Chombo Redondo, Amri
Kiemba Athumani, Abdallah Omar Seseme, Ramadhani Singano Yahya, Uhuru Selemani
Mwambungu, Mrisho Khalfan Ngassa, Mwinyi Kazimoto Mwetula na Salim Abdallah
Kinje na washambuliaji Abdallah Juma, Daniel Akuffo, Felix Mumba Sunzu, Edward
Christopher Shija, Haruna Athumani Chanongo na Emmanuel Arnold Okwi.
Waliobaki Dar es Salaam ni Haruna Moshi ‘Boban’ anayesumbuliwa
na maumivu ya misuli, Haruna Shamte, anayeumwa goti, Kigi Makassy anayeumwa goti
pia, Shomari Kapombe anayesumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu na Juma Said
Nyosso anayetumikia adhabu ya kadi (tatu za njano).
Simba bado inaongoza Ligi Kuu kwa pointi zake 18, baada ya
kucheza mechi nane, ikifuatiwa na Azam yenye pointi 17, baada ya kucheza mechi
saba, wakati Yanga inayocheza mechi ya nane na Ruvu Shooting leo Dar es Salaam ni
ya tatu kwa pointi zake 11.