Hans Poppe |
Na Mahmoud Zubeiry
SIMBA SC wamesema kwamba sasa inatosha kufanywa wajinga,
wanataka kuwapa somo na Yanga ili wajue kwamba wao siyo klabu ya kuchezewa.
Kufanya wajinga kivipi na wanataka kutoa somo gani?
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya klabu ya Simba, Zacharia
Hans Poppe amesema kwamba wanakusanya vielelezo vya vyombo vya Habari juu ya
mwenendo mzima wa sakata la beki Mbuyu Twite na kuvipeleka Mahakama ya
Usuluhishi (CAS) ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Kisa nini? Hans Poppe amesema ni ukimya wa TFF kutowapa rasmi
taarifa ya hukumu ya pingamizi lao la Twite katika klabu ya Yanga na pia
kushindwa hata kusimamia hukumu waliyotoa.
Lengo nini? Hans Poppe amesema wanaamini kesi hiyo ikifika
CAS, Twite atafungiwa kucheza soka na hata Yanga wataadhibiwa pia kwa kufanya
kitendo kisicho cha kiungwana, kumsajili mchezaji ambaye tayari alikwishaini
mkataba na klabu nyingine.
“Sisi kama Simba hadi leo hatuna taarifa rasmi kutoka TFF juu
ya hukumu waliyotoa katika kikao chao cha Kamati ya Sheria, Maadili na Hadhi za
Wachezaji. Tumekuwa tukisikia tu kupitia vyombo vya habari, wakati sisi tuliwasilisha
pingamizi letu kwa maandishi, naamini huu si utendaji sahihi,”alisema Hans
Poppe.
Pamoja na hayo, Mwenyekiti huyo ambaye ni Kapteni wa zamani
wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ), amesema kwamba TFF pia iliamuru Yanga
wawe wamekwishalipa fedha ambazo Twite alichukua Simba hadi kufika Oktoba 3,
mwaka huu, lakini sasa mwezi huo unaelekea ukingoni na klabu yao haijalipwa.
“Tunashindwa kuelewa hii ina maana gani, kwa sababu hukumu
wametoa wao, na wao ndio wenye wajibu wa kusimamia utekelezaji wake, lakini
hadi leo Yanga hawajalipa na TFF pamoja na Kamati ya Sheria na Maadili wamekaa
kimya, sasa sisi tunachukua hatua ambayo baadaye tusije kulaumiana,”alisema
Hans Poppe.
Alisema anashangaa TFF wamekuwa wepesi katika kusimamia na
kutekeleza adhabu za Simba, kwa mfano barua barua ya hukumu ya mshambuliaji
wao, Emmanuel Okwi kufungiwa mechi tatu waliipata mapema tu baada ya kikao cha
Kamati cha Ligi kupitia ripoti ya mechi ambayo Mganda huyo aliadhibiwa.
“Tumekwishawaandikia barua ya kuwaomba hati ya hukumu siku
nyingi, lakini bado hadi leo hawajatupa, sasa tunashindwa kuelewa nini lengo
lao, tunafikiria wanajua tukikata rufaa CAS tutashinda, sasa wamejawa hofu na
wanaogopa kutoa hukumu kwa maandishi,” alisema Hans Poppe.
Septemba 10, mwaka huu Kamati ya Sheria na Hadhi za
Wachezaji, chini ya Mwenyekiti wake, Alex Mgongolwa ilitoa maamuzi ambayo
hayakuwaridhisha walalamikaji, Simba SC juu ya Twite na Yondan na sasa wanataka
kulipeleka suala hilo CAS.
Kamati hiyo, iliitaka Simba kuthibitisha madai yake ya
kuingia mkataba na Yondan na kuwasilisha upya malalamiko yake kwenye kamati
hiyo.
“Kwa mujibu wa Ibara ya 44 (3) ya Kanuni za Uhamisho wa
Wachezaji za TFF, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Kevin Yondan,
hivyo ni mchezaji wake halali.
Kwa vile Simba imesema mchezaji huyo vilevile alisaini
mkataba na klabu yao, imetakiwa kupitia mamlaka nyingine kuthibitisha hilo, na
baada ya uthibitisho iwasilishe malalamiko yake kwenye Kamati ya Sheria,
Maadili na Hadhi za Wachezaji, au mamlaka zozote za kisheria kwa mujibu wa
madai/lalamiko husika,”alisema Mgongolwa.
Kuhusu suala la Mbuyu Twite, Mgongolwa alisema kwamba kwa
mujibu wa Ibara ya 18(3) ya Kanuni za Hadhi na Uhamisho wa Wachezaji wa
Kimataifa za FIFA, Yanga ilifuata taratibu zote katika kumsajili Mbuyu Twite,
hivyo ni mchezaji wake halali.
Hata hivyo, alisema kwa vile Yanga imekiri kuwa mchezaji huyo
alichukua dola 32,000 za Simba na kukiri kuzirejesha, kwa msingi wa kanuni ya
Fair Play, Kamati imeipa Yanga siku 21 iwe imelipa fedha hizo Simba.
Wajumbe sita kati ya saba waliopo walihudhuria kikao hicho
chini ya Mwenyekiti Alex Mgongolwa. Wajumbe hao ni Hussein Mwamba, Imani
Madega, Ismail Aden Rage, Llyod Nchunga na Omari Gumbo.
Siku 21 walizopewa Yanga kurudisha fedha za Twite alizochukua
Simba, zilimalizika Oktoba 3, siku ambayo watani hao wa jadi katika soka ya
Tanzania, walimenyana katika mchezo wa Ligi Kuu, mzunguko wa kwanza Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam na kutoka sare ya 1-1.
Simba walitarajia TFF ingeikata Yanga fedha hizo katika
mapato yake ya mechi hiyo, lakini hawakufanya hivyo na hadi leo pia bado
hawajalipwa na ndiyo maana wanaamua kupeleka vielelezo hivyo CAS.
Mgongolwa aliwahi kuiambia BIN ZUBEIRY kwamba,
kutokana na Yanga kushindwa kutekeleza agizo, hilo amemuagiza Katibu wa TFF
aitishe kikao kingine cha Kamati hiyo ili kujadili hatua ya kuichukuliwa klabu
hiyo kuwa kukaidi agizo hilo.
Hata hivyo, yapata wiki mbili sasa tangu Mgongolwa amesema
hivyo na hakuna dalili za Kamati yake kukutana kumaliza mgogoro huo.